Mashindano ya Umoja wa shule za Sekondari nchini
Tanzania (UMISSETA) 2018 yameendelea kutimua vumbi leo hii kwa michezo
mbalimbali kuweza kupigwa ambapo katika mtanange wa mpira wa miguu hatua ya
robo fainali wavulana, Timu ya mkoa wa Mwanza imeendeleza ubabe wa kutopoteza
mchezo ata mmoja baada ya kuifunga timu ya mkoa wa Pemba kutoka Tanzania
Visiwani kwa jumla ya mabao 3-1 katika hatua ya robo fainali,mtanange uliopigwa
katika uwanja wa Nsumba Sekondari jijini Mwanza.
Katika hatua nyingine Timu ya mkoa wa Tanga
imefanikiwa kufuzu kuingia katika hatua ya Nusu Fainali baada ya kuiondosha
Timu ya mkoa wa Mara kwa jumla ya mabao 2-0, mchezo uliochezwa katika uwanja wa
chuo cha ualimu Butimba ambapo kwa matokeo hayo sasa timu hiyo itakutana na
timu ya mkoa wa Dar es Salaam ambayo ilifanikiwa kuitupa nje timu ya Mkoa wa
Iringa kwa magoli 2-0 katika hatua ya robo fainali.
Hatua ya nusu fainali itaendelea tena kesho kwa
michezo hiyo kupigwa mida ya jioni katika uwanja wa chuo cha ualimu Butimba
ambapo Tanga watacheza na Dar es Salaam kuanzia saa 9 alasiri na Mwanza
watachuana na Geita kuanzia mida ya 10 jioni.
Kwa upande wa Michezo ya wasichana Mpira wa miguu
timu ya mkoa wa Mbeya ambayo ndio ilidhaniwa kuwa timu tishio katika mashindano
hayo ilijikuta ikutupwa nje kwa mikwaju ya penati 3-1 na timu ya mkoa wa
Tabora, wakati Dar es salaam wakiichachafya timu ya mkoa wa Kagera kwa magoli 3-0.
Aidha katika mchezo wa netiboli hatua ya robo
fainali timu za mkoa wa Dar es salaam, Tanga, Mwanza na Morogoro zimetinga
katika hatua ya nusu fainali baada ya DSM kuifunga Tabora kwa magoli 55 kwa 27,
Tanga kuifunga Mara kwa magoli 40 kwa 33, Mwanza kuifunga Geita kwa magoli 54
kwa 46 na Morogoro kuifunga Singida kwa magoli 64 kwa 19.
Na katika mchezo wa mpira wa mikono (Handball) kwa
upande wa wasichana timu ya mkoa wa Songwe itaumana na Timu ya mkoa wa Mbeya
wakati Morogoro ikimenyana na timu ya mkoa wa Mara, huku wavulana wao Dar es
salaam itakuwa na kibarua dhidi ya mkoa wa Tanga wakati Mwanza ikicheza na
Unguja.
0 comments:
Post a Comment