Ndugu Waandishi wa Habari,Sekretarieti ya TFF, Watanzania
wote wanaotuangalia na kutusikiliza,mabibi na mabwana habari za asubuhi.
Naomba nianze kwa
kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana mahali hapa siku ya leo
tukiwa wazima wa Afya,Lakini pia nichukuwe nafasi hii kuishukuru Serikali ya
awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dr.Joseph
Pombe Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata katika uendeshaji wa mpira wa
miguu, nimekuwa karibu sana na Serikali kuhakikisha juhudi zetu za kuendeleza
mpira zinafanikiwa kwa kasi kubwa sana na mafanikio ya ujio wa Rais wa FIFA ni
kielelezo cha karibuni kuonyesha ushirikiano mkubwa tunaoupata toka kwa
Serikali hasa Waziri mwenye dhamana ya michezo Mh.Dr,Harrison Mwakyembe na timu
yake.
Lakini niwashukuru kwa nafasi ya kipekee ndugu zangu
Waandishi wa Habari kwa kazi kubwa mnayoifanya kuhabarisha umma kuhusu habari
za mpira wa miguu,Pia pongezi zenu kwa kazi nzuri mliyoifanya wakati wa ujio wa
FIFA, mlifanya kazi kubwa sana kutangaza ziara ya Rais wa FIFA, mmetupa heshima
kubwa sana.
Ndugu zangu, leo nitaongelea mambo makubwa mawili ili waTanzania
wapate kufahamu kinachoendelea katika mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.
Moja nitaongelea kuhusu mambo ambayo tumeyafanya kwa
kipindi cha miezi saba nilichokuwepo madarakani lakini la pili ni mambo
yanayoendelea sasa hivi kwenye Shirikisho.
MAMBO AMBAYO TUMEYAFANYA
KWA MIEZI SABA TOKA TUINGIE MADARAKANI
HALI NA SHUGHULI ZA TAASISI
Kwa Mazingatio ya Utekelezaji Makini na wa Maendeleo wa Shughuli za Taasisi
Tulitambulisha Muelekeo na Dira ya TFF ambapo Kazi iliyo Mbele yetu ni Kuzitoa
na Kuimarisha Utambuzi na Utekelezaji wake. Sasa ni wakati Tunajiandaa Kutoa
baadhi ya Mipango yetu na kutoa Dira za Utekelezaji wake. Pamoja na Mipango
hiyo Bado TFF tumekuwa Tukitekeleza Shughuli za Mpira katika Mgawanyiko wake na
labda kwa kifupi kugusia Miongoni mwake.
Mashindano.
Tumeendesha mashindano mbalimbali kwa ufanisi mkubwa
yakiwemo mashindano ya Azam Sports Federation Cup, Ligi ndogo ya Wanawake kwa
ajili ya kupata timu za kupanda daraja,Ligi Kuu ya Wanawake hatua ya makundi na
hatua ya nane bora inayoendelea,Mashindano ya soka la ufukweni kwa timu za vyuo
vikuu,Mashindano ya kimataifa ya soka la
ufukweni yajulikanayo COPA DAR ES SALAAM.
Azam Sports
Federation cup;
Mashindano hayo kwa msimu huu 2017/18 tumeyaendesha kwa
ufanisi na umakini mkubwa tofauti na huko nyuma kwa kuhakikisha upangaji wa
ratiba umekuwa wa wazi usio na upendeleo wowote ule hivyo kupunguza malalamiko,jambo
lingine tulihakikisha timu zote zinapata stahiki zao kwa wakati na kiwango kilichopangwa,kadiri
tunavyoelekea hatua za mwisho wa mashindano tutahakikisha changamoto zote
zilizojitokeza huko nyuma tunakabiliana nazo na kuzitatua ili kuhakikisha
mashindano hayo yanaisha vizuri.
Ligi kuu ya Wanawake;
Mwaka huu tulianza kucheza Ligi ndogo ya Wanawake kutafuta
timu za kupanda Ligi Kuu ya Wanawake katika vituo vya Dar es salaam na
Dodoma,ikafuatiwa na Ligi ya Wanawake katika kituo cha Arusha na Dar es Salaam
ili kupata Timu 8 za kucheza hatua ya Nane bora ya Ligi hiyo.
Katika hatua ya makundi, TFF ilizigharamia timu zote kwa asilimia 100 kuanzia malazi, usafiri,
chakula, gharama za maadalizi ya timu na nauli ya kwenda na kurudi,ikiwa ni
mara ya kwanza katika historia ya mpira wa miguu wa Wanawake kwa TFF kugharamia
kwa kiwango hiki.
Katika hatua ya Nane bora ya Serengeti Lite Women Premier League vilabu
vyote vilishapewa fedha zao kwa ajili ya hatua ya kwanza ambayo imesimama
kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake(Twiga Stars) ambayo inajiandaa
na mashindano ya kufuzu michuano ya Afrika kwa Wanawake ambapo tayari timu ya Taifa
ipo kambini ikijiandaa na mchezo huo dhidi ya Zambia.
Taasisi iliendesha kwa
mafanikio makubwa mashindano ya soka la ufukweni (Copa Dar es Salaam) kwa
kuzialika timu za Uganda, Malawi, Zanzibar na wenyeji Tanzania bara ambazo
tulizigharamia malazi, chakula na usafiri wa ndani.
PROGRAMU
ZA TIMU ZA TAIFA
Toka tumeingia
madarakani, tumekuwa tunafanyia kazi program mbalimbali za maendeleo ya Timu za
Taifa.
Taifa
Stars
Tumekuwa tukiendelea na
program mbalimbali za Timu ya Taifa za kuhakikisha inafuzu Fainali za kombe la
mataifa Afrika 2019.
Kuhakikisha hili Taifa
Stars ilicheza na Benin, Malawi, Botswana na wiki hii tunacheza na Algeria
pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika kalenda ya mechi za
kimataifa ya FIFA.
Ili kuongeza hamasa ya
wachezaji tumeongeza posho ya ndani kwa asilimia 100 na asilimia 50 kwa posho
za nje.
Kilimanjaro
Stars
Timu yetu ya Tanzania
bara ilishiriki mashindano ya CECAFA yaliyofanyika nchini Kenya mwezi Desemba
2017, mbali na kushiriki ili ichukuwe kombe sababu nyingine ilikuwa ni
kuendelea kupata mechi nyingi za kimataifa.
Timu ilicheza dhidi ya
Rwanda, Kenya, Zanzibar na Libya, Tunaamini kwa wachezaji vijana waliokuwa
sehemu ya kikosi hicho imewajengea uwezo katika soka la kimataifa.
Timu
za Taifa za Vijana
Katika eneo hili tumekuwa na mpango wa muda mrefu kuhakikisha
vijana wa timu zetu za Taifa za miaka chini ya 23, 20, 17 na 13 zinakuwa na
maandalizi bora na kwa kuanzia toka tuingie madarakani tumekuwa na kambi za
timu za vijana kila mwezi kwa kuwakutanisha siku 14 za mazoezi na kuwatafutia mechi
za kirafiki za kimataifa.
Timu
ya U23
Timu ya Taifa chini ya
miaka 23 ambayo ni kikosi cha pili cha timu ya Taifa kimeshaitwa kambini mara
kadhaa na tumethibitisha kushiriki mashindano ya Olimpiki ambayo fainali zake
zitafanyika nchini Japan, lengo ikiwa ni
kuhakikisha tunawapatia vijana hawa mechi nyingi za kimataifa ili wawe tayari.
Timu
ya Vijana U20
Timu ya Vijana U20
ambapo jana ilicheza na Morocco na Jumatano itacheza na Msumbiji, ikiwa ni
maandalizi ya mechi dhidi ya timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Congo(DRC) ikiwa ni mchezo wa kufuzu fainali za Vijana Afrika
chini ya miaka 20.
Timu
ya Vijana U16
Timu hii nayo imekuwa
ikiingia kambini kila mwezi na hata sasa hivi ninavyozungumza na nyinyi, timu
hii ipo kambini ikijiandaa kwa mashindano ya CECAFA na tunafanya jitihada za
kuhakikisha inapata mechi mbili za kirafiki za kimataifa kabla haijaenda
Burundi.
Timu hii ndiyo ambayo
itashiriki fainali za Afrika chini ya miaka 17 zitakazofanyika hapa nchini mwaka
2019.
Baada ya kutoka Burundi
itakuwa na program maalum kwa ajili ya kujiandaa kwa mashindano mengine ya
kufuzu AFCON U17, 2019 ambayo yatafanyika nchini mwezi Agosti ambayo lengo ni
kupata mwakilishi wa CECAFA na vijana wetu watashiriki kama wenyeji. TFF
imeamua kushirikisha Timu yenye Umri mdogo zaidi kwa u17 bila ya kujali Matokeo
zaidi ya Ujenzi wa timu kwa kuandaa timu moja katika matukio yote haya ili
kuiweka tayari kwa Mashindano ya u17 ya 2019 mwakani ambapo vijana hawa ndio
watakuwa rasmi u17
Timu
ya Vijana ya U13
Timu ya Vijana ya U13 katika
kutafuta namna ya Kuwaimarisha vijana
hawa baada ya Utambuzi na Uteuzi wa timu imepata nafasi ya kushiriki mashindano ya kirafiki ya vijana
chini ya miaka 13 yatakayofanyika nchini Ubelgiji mwezi Agosti 2018,Tayari
orodha ya kwanza ya wachezaji 69
waliopatikana katika mashindano ya shule za msingi (UMITASHUMITA) ipo
TFF na idara ya ufundi inaandaa utaratibu wa kuwaita pamoja na kupata michezo
ya kirafiki dhidi ya Zanzibar kwa ajili ya kupata kikosi cha pamoja cha
Tanzania.
Timu
ya Taifa ya Wanawake U20
Tumeanza kuandaa kikosi
cha Vijana cha timu ya taifa ya Wanawake U20 ili kuwa na kikosi bora cha Twiga
Stars kilichoandaliwa kwa muda mrefu na tayari ilishacheza michuano ya kufuzu
fainali za vijana za Afrika chini ya miaka 20 na kutolewa na Nigeria.
Baadhi ya wachezaji wa
timu hii wamepandishwa kikosi cha wakubwa na sehemu kubwa wanacheza Ligi Kuu ya
Wanawake kupitia vilabu mbalimbali.
Tutaendelea na
utaratibu wa kuwaita kambini kila wakati kutakapokuwa na nafasi ili kuzidi
kuimarisha kikosi.
Twiga
Stars
Kikosi cha Twiga Stars kimeingia
kambini kwaajili ya maandalizi ya mashindano ya kufuzu fainali za Africa kwa
Wanawake zitakazofanyika nchini Ghana baadaye mwaka huu.
Twiga Stars inakabiliwa
na mchezo dhidi ya Timu ya Taifa ya Zambia utakaochezwa Aprili 4,2018 Uwanja wa
Taifa na marudiano kuwa Aprili 8,2018 nchini Zambia.
MAPATO NA
MATUMIZI
MAPATO
Katika
kipindi cha miezi Saba(7),Shirikisho limefanikiwa kukusanya kiasi cha Tzs 3,670,397,199.00 kutoka katika vyanzo
vyake mbalimbali ambavyo ni pamoja na
mapato kutoka kwa wadhamini Tzs 2,295,472,151
sawa na 62.5% ya mapato yote,
makusanyo ya viingilio uwanjani Tzs 378,139,866
sawa na 10.3%. 27.2% ilitokana na
Fedha kutoka CAF na FIFA.
MATUMIZI
Katika
kipindi hiki Shirikisho lilitumia kiasi cha Tzs 3,752,001,171.00. Sehemu kubwa ya matumizi yalielekezwa kwenye
usimamizi wa ligi mbalimbali pamoja na kuandaa timu za taifa ambapo jumla ya
Tzs 2,409,150,732 sawa na 64% ya matumizi yote zilitumika.
Asilimia
36 ya Fedha zilizobaki ilitumika kulipia madeni ya Taasisi, Kulipa mishahara ya
wafanyakazi, kusaidia mikoa katika maeneo ya miundo mbinu, kuwajengea uwezo
wafanyakazi pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali.
Kama
Rais wa TFF sijapokea HOJA wala USHAURI wala MAPENDEKEZO yoyote kutoka kwa
Wajumbe wangu katika Ngazi zote kuhusiana na Matumizi ya Taasisi, Nasikitika
kama kuna anayedai amehoji sijui wapi kwa kuwa kama Rais sijapokea hoja yoyote
wala kuwasilishwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji iliyopita ambayo Taarifa
ya Kamati ya Fedha iliwasilishwa nakupokelewa na kupitishwa na Kamati ya
Utendaji.
MADENI
Katika
kipindi hiki,Shirikisho lilianza zoezi la kutathmini madeni iliyoyarithi kutoka
kwenye Uongozi uliopita, ambapo deni hilo linafikia Tzs 2,172,000,000 linalodaiwa na watoa huduma mbalimbali,
wafanyakazi,wachezaji na makocha.
Asilimia
kubwa ya deni hili lilitokana na malimbikizo ya deni la TRA, Workers
Compensation Fund na NSSF ambalo lililimbikizwa kwa zaidi ya miaka miwili.
Shirikisho
lilifanikiwa kulipa deni lote la michango ya wafanyakazi NSSF jumla ya Tzs
88,000,000 zilizokuwa hazijalipwa kipindi cha miaka miwili, na lilifanya
majadiliano na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu ulipaji deni la kodi linalofikia
Tzs 1,077,000,000, ambapo jumla ya Tzs 315,000,000 zimelipwa na kiasi kilichobaki tumekubaliana
kitalipwa kwa awamu kadhaa mpaka deni lote litakapomalizika.
Pia shirikisho
limefanikiwa kupunguza mishahara kwa wafanyakazi kutoka Tzs 85,063,092.00
mpaka kufikia 50,000,000.00 baada ya kupunguza idadi ya wafanyakazi kutoka 44
mpaka 21.
Baada ya
kuingia madarakani tulifanya majadiliano na makocha wa timu za Taifa kuhusu
uhalisia wa malipo yao na kufanikiwa kuokoa zaidi ya dola laki mbili(USD
200,000) kwenye mikataba yao na fedha zilizookolewa zitasaidia shughuli nyingine
za mpira wa miguu.
UFUNDI
1. Kliniki
iliyoendeshwa na Kocha PiaSundhage kutoka Sweden
2. Kozi ya ngazi ya
awali ya makocha wa mpira wa miguu
ilifanyika katika mikoa
ya Kigoma,Songwe, Lindi, Morogoro na Pwani
3. Kozi ya ngazi ya
kati ya makocha wa mpira wa miguu
Ilifanyika katika mikoa ya Kigoma mara mbili,
Manyara na Morogoro.
4.Grassroot & Live
your goal project
Kozi hii ilifanyika
katika mikoa ya Lindi ambapo washiriki walitoka katika mikoa ya Lindi na
Mtwara.
Pia kozi nyingine ilifanyika katika mkoa wa
Mbeya ambapo washiriki walikuwa ni kutoka katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Katavi,
Songwe na Rukwa
Aidha hii kozi
ilifanyika Kigoma na kushirikisha washiriki wa mikoa ya Kigoma na Tabora.
5.Mafunzo ya awali ya Utawala
mikoani
Kuna kozi ya utawala na masoko iliyofanyika
Dar es Salaam ili kuwaongezea watu wa masoko uwezo wa kuwavutia wadhamini.
6.Mafunzo ya waamuzi
Mafunzo ya waamuzi wa FIFA na Waamuzi wa
ngazi ya juu yalifanyika mara tatu jijini Dar es Salaam.
7. Kozi ya kupandisha
daraja kwa Waamuzi
Kozi hii ilifanyika
mara mbili katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.
8. Ziara za
Mafunzo na kubadilishana uzoefu
Zilifanyika ziara mbalimbali za Waamuzi wetu
za kubadilishana uzoefu katika nchi mbalimbali.
9. Mpango wa ugawaji wa vifaa
vya vijana na mafunzo
Tulipoingia
madarakani tulikuta uongozi uliopita wameshanunua mipira na imekaa stoo, katika
kutekeleza azma ya maendeleo ya vijana ili tuwe na timu za Taifa imara
Shirikisho limegawa mipira (100 kwa kila Mkoa) saizi 4 na 3 kwa Mikoa yote ya
Tanzania Bara na Zanzibar, Mikoa imepewa vifaa vya kufundishia (cones and
markers) ili vijana wapate fursa ya kuonesha na kuendeleza vipaji vyao kwa
maslahi ya Mpira hapa nchini.
Uzinduzi wa
zoezi hili ambalo linategemewa kuwa endelevu lilifanyika Uwanja wa Taifa Agosti
3, 2017.
Rais wa TFF
aliwakabidhi wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa niaba ya Mikoa yao kwenye Kanda
husika, Kwa upande wa Zanzibar Katibu Mkuu wa ZFA alikabidhiwa mipira hiyo kwa
ajili ya Mikoa ya Zanzibar.
MASOKO
NA HABARI
Tumeendelea
kuongeza wadhamini katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha Taasisi inanufaika
na bidhaa zake.Lakini pia tumeendelea kuimarisha idara ya habari kwa
kuwanunulia nyezo za kufanyia kazi.
UTAWALA
BORA
Katika kipindi hiki cha
Miezi saba nimesimamia eneo hili kwa uadilifu mkubwa, Kamati zimekuwa
zinakutana kabla ya vikao vya Kamati ya Utendaji ili kuhakikisha kila mmoja
anashirikishwa.
Mfano, Wakati
nilipokuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha,kwa miaka 4 nilikaa kikao kimoja cha
Kamati ya Fedha,Katika Utawala wangu aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha
ndani ya miezi saba ameitisha vikao visivyopungua vitano.
Nilimuagiza Kaimu
Katibu Mkuu kuhakikisha kila Kamati ya Fedha inapohitaji kukutana ahakikishe
inakutana na Mtendaji Mkuu amekuwa anatekeleza.
Na kwa sababu nafasi ya
Makamu wa Raisi Kikatiba ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango, basi
hata mazungumzo ya Mkataba wa Udhamini wa Ligi Kuu msimu 2018/2019 yeye ndiye
aliyekuwa anasimamia.
Nimekuwa nafanya hivi
ili Taasisi iendeshwe kwa uwazi na kushirikisha kila mmoja,Na nimeendelea
kusisitiza kuwa mapato ya matumizi ya Taasisi yatatolewa kwenye vyombo vya
Habari ili yawe wazi kwa umma.
SEKRETARIETI
YA TFF
Toka tuanze kuunda
sekretarieti tumeajiri Wakurugenzi Watatu na Meneja mmoja na wote hawa
waliajiriwa na Kamati ya Utendaji, Ofisi ya Katibu Mkuu haijawahi kuajiri
mfanyakazi hata mmoja kufikia sasa.
Nafasi ambayo
haijajazwa ni nafasi ya Katibu Mkuu ambako Ndugu Kidao Wilfred bado anakaimu.
Kwanza nikiri kazi
nzuri inayofanywa na mtendaji mkuu aliyekuwepo katika kuhakikisha Taasisi
inapiga hatua kwa kasi kila ninapokutana na watendaji wakuu wa FIFA, CAF na
CECAFA wamekuwa hawasiti kunimwagia sifa kwa kuwa na sekretarieti mahiri
iliyobadilika katika kufanyia kazi changamoto za Taasisi.
Raisi wa FIFA alisema
anaona mabadiliko makubwa ya hatua tunazochukuwa, Lakini Katibu Mkuu wa FIFA
alisema nina Sekretarieti ya Vijana wenye hali, nguvu na maono ya kuipeleka
Taasisi mbele huo ndio ujumbe wao.
Nimeyasema haya kuwahakikishia
nikiwa msimamizi wa sekretarieti, mambo yote ambayo Kaimu Katibu Mkuu amekuwa
akiyafanya ni maelekezo yangu au utekelezaji wa maamuzi halali ya kamati ya
Utendaji, Kwahiyo nichukuwe fursa hii kupongeza kasi ya sekretarieti katika
kusimamia mambo mbalimbali.
AJIRA
Katika kipindi changu
cha uongozi (Kamati ya Utendaji) kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu Mkuu
tumeweza kupunguza wafanyakazi kutoka Wafanyakazi 44 tuliowakuta wakati naingia
madarakani hadi kufikia 21,Ni hatua kubwa na tunafanya upembuzi makini kabla
hatujaanza kuajiri watu tuwe na mahitaji stahiki.
KATIBU
MKUU
Kumekuwa na maneno
mengi juu ya nafasi ya Katibu Mkuu wa Shirikisho, Ndugu zangu wakati naanza
kazi niliona ni muhimu nafasi hii ikaimishwe kwa mtu anayelijua shirikisho
vizuri na ambaye sina shaka na uwezo wake,Sifa zote hizi alikuwanazo KIDAO
WILFRED na wajumbe wa Kamati ya utendaji chombo ambacho kinahusika nakupitisha
kilibariki awe Kaimu Katibui MKuu.
Kutoka nje ya Ofisi na kukaimu
hii siyo mara ya kwanza,wakati Ndugu Tenga anashinda Uraisi alimuomba Bi.Lina
Kessy ambaye alikuwa mtumishi wa Serikali kuwa Mratibu wa Ofisi, nafasi
iliyokuwa kama Mkuu wa sekretarieti wakati huo.
Hata wenzetu wa CAF,
Rais ndiye anayepeleka jina bila kujali Mchakato utakavyokuwa kwa maana
wanaweza wakatangaza au wasitangaze,na hata Katiba ya TFF inahitaji Rais wa TFF
atoe mapendekezo ya Katibu Mkuu ili Kamati ya Utendaji ijadili, haya yanafanyika
kwa sababu Rais kama msimamizi wa Sekretarieti anafanya kazi kwa karibu sana na
Katibu Mkuu hivyo FIFA wanahitaji watu hawa wawe wanaoweza kufanya kazi kwa karibu
sana,ndipo Rais wa TFF anapopewa kipaumbele cha mtu wa kufanya naye kazi
kwakuwa ndio nguzo ya Taasisi kwakuwa Rais ndio mkuu wa Taasisi na Katibu Mkuu
ndio mkuu wa Sekretarieti.
Lakini pamoja na yote hayo
bado nilikuwa napeleka ajenda ya Ajira kwenye Kamati ya Utendaji ili
kushauriana njia bora ya kupata Katibu Mkuu kwa maslahi mapana ya Mpira wa
Miguu na siyo mtu.
Niwahakikishie kikao
kijacho cha kamati ya Utendaji kitaamua njia sahihi ya kupata Katibu Mkuu na
tutahakikisha tunakuwa na Katibu Mkuu ndani ya muda mfupi ujao.
Mipango
Mbalimbali
Tumekuwa katika Ujenzi
wa Mipango Mbalimbali kama nilivyoainisha kwenye Ilani yangu ambapo Katibu Mkuu
amekuwa Kiungo muhimu katika kunisaidia kwenye Ujenzi wa Mipango yangu hiyo
lakini kwa bahati Mbaya Kaimu Katibu Mkuu Kidao amekuwa kwenye wakati mgumu
kutokana na kuandamwa na Maneno na Vitendo vinavyolenga na kufanikisha
kumkwamisha na kumkosesha mazingira bora na rahisi ya kufanyia kazi zake na
hivyo imekuwa ni atahri kwa TFF kwa Baadhi ya Mipango yake kuwa inakwama kutoka
Mpaka sasa na hiyo ni athari kwa Mpira wetu kwa Ujumla.
Ndugu
zangu jambo la pili ambalo nimeona niligusie ni jinsi vyombo vya maamuzi vya
TFF vinavyofanya kazi,
Ndugu waandishi, TFF
inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba yake ya mwaka 2013 na kufanyiwa marekebisho
mwaka 2015. Katiba hii inataja Kamati ya Utendaji itaundwa na Wajumbe wafuatao;
1. Rais
2. Makamu wa Rais
3. Wajumbe 13 kutoka
kanda zilizotajwa ibara 32 ya katiba ambazo ni Kanda namba 1-Kagera na Geita
Kanda namba 2- Mara na
Mwanza
Kanda namba 3-
Shinyanga na Simiyu
Kanda namba 4- Arusha
na Manyara
Kanda namba 5- Kigoma
na Tabora
Kanda namba 6- Katavi
na Rukwa
Kanda namba 7- Mbeya,
Iringa na Songwe
Kanda namba 8- Njombe
na Ruvuma
Kanda namba 9- Lindi na
Mtwara
Kmada namba 10- Dodoma
na Singida
Kanda namba 11- Pwani na
Morogoro
Kanda namba 12-
Kilimanjaro na Tanga
Kanda namba 13- Dar es
Salaam
4. Wajumbe wawili
wanowakilisha vilabu vya Ligi Kuu
5.Mwenyekiti wa Chama
cha Soka ya Wanawake.
6. Mwenyekiti wa Kamati
ya Tiba
7. Wajumbe wawili wa
kuteuliwa na Rais wa TFF.
Rais wa TFF amepewa
nafasi za kuteua wajumbe wawili wa kamati ya Utendaji ili kumsaidia kufanya
kazi na watu ambao wanajua muelekeo wake lakini ambao anaamini watamsaidia
kwenye maeneo mbalimbali katika Taasisi.
Kamati ya Utendaji
inafanya kazi na vyombo mbalimbali ambavyo ni Kamati ndogondogo, Bodi ya Ligi
na Kamati za Kisheria pamoja na Kamati za Uchaguzi.
Kamati
Ndogondogo;
- Fedha na Mipango
- Mashindano(Kamati ya Tuzo na Soka la Ufukweni)
- Ufundi na Maendeleo
- Vijana
- Wanawake
- Waamuzi
- Katiba, Sheria, na Hadhi za wachezaji.
- Tiba
- Ukaguzi (ambayo yenyewe ni kama Kamati huru)Kamati za Kisheria;
- Nidhamu
- Rufani ya Nidhamu
- Maadili
- Rufani ya Maadili
Kamati
za Uchaguzi;
- Uchaguzi
- Rufani ya Uchaguzi
Ufanyaji wa kazi wa
Kamati hizi umeelezewa katika Katiba ya TFF kwa maana Kamti za Kisheria
zinajitegemea huwa haziingiliwi kwenye maamuzi yake.Ingawa vikao vyake vyote
huwa vinaratibiwa na ofisi ya Katibu Mkuu.
Kwahiyo maamuzi ya
Kamati hizi huwa ni ya kujitegemea hivyo watu wote ambao wamekuwa wanahukumiwa
na Kamati hizi ni vyema wakawa wanajua utaratibu wa Kamati zinavyofanya kazi.Na
mimi binafsi nimeendelea kuheshimu Kamati zifanye kazi bila kuingiliwa na mtu
yoyote vile.
Ndiyo maana wakati
nachaguliwa niliahidi kusimamia Taasisi kwa uadilifu mkubwa bila kumuonea aibu
mtu yeyote, wala kumuogopa mtu na hii ni katika kuunga mkono juhudi za Raisi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
kupambana na uchafu wa aina zote katika
serikali,Nami nimeamua kusafisha Taasisi kama nilivyoahidi wakati wa Kampeni za
uchaguzi ulioniweka madarakani,niseme wazi hakuna mtu asiye muadilifu atabaki
katika mpira,Na nimpongeze Kaimu Katibu
Mkuu wangu kwa kusimamia kwa ujasiri mkubwa usimamiaji wa maagizo yote halali
ya Kamati mbalimbali,Amekuwa anasimamia bila uoga bila kujali anavyosakamwa kwangu
linanipa faraja sana.
Tumekuwa tunachukuwa
hatua katika kila eneo tumeshaanza kuchukuwa hatua kwa wizi wa Mapato ya milangoni,
kuna viongozi wamefungiwa,hatukuishia hapo tayari viongozi walioghushi leseni
za usajili wamefungiwa,Hiyo yote ikiwa ni kuonesha sina masihara hata kidogo
kwenye kuhakikisha mpira unakuwa sehemu ya watu waadilifu.
FIFA walituma Timu ya
Uchunguzi(Investigation Team) kuangalia yale yote yaliyofanyika toka mwaka 2013
mpaka mwaka 2017,Timu ilikaa nchini kwa takribani wiki mbili ikifanya kazi kwa
karibu na Ofisi ya Katibu Mkuu,Yaliyogundulika yameacha doa kubwa na walitoa
Ripoti na Maelekezo ya mambo ya kuyafanyia kazi na ya kuchukulia hatua.
Masharti yote haya
yaliambatana na kuzuiwa kwa fedha zetu za miradi nia na wenzetu wachache,
Lakini tumekosa pesa zinazoitwa Operation Cost ikiwa ni shinikizo la Dola
Milioni Tatu ambazo tulipaswa kulipwa toka mwaka 2015-2018.
Karibia nchi zote
Duniani zimenufaika kwa kupata pesa hizi, isipokuwa Tanza kuhakikisha tunatekeleza
masharti ya FIFA, Hivyo tulipopata ripoti tumeamua kutekeleza kwa asilimia mia
moja maagizo yote ya FIFA. Haya yanayotokea ni Miongoni mwa Matokeo ya
Utekelezaji wa Taarifa za Wakaguzi wa TFF na Wakaguzi na Timu ya Uchunguzi
kutoka FIFA. Jambo hili limepitia Hatua stahiki kwa Mujibu wa Taratibu
zinazohusiana na Taarifa za kiUkaguzi na wahusika wameshirikishwa ipasavyo na
Utetezi wao walipeleka kwenye Kamati husika ya Ukaguzi miezi iliyopita baada ya
kutakiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu.
Niseme tu unaposafisha
Taasisi kuna gharama zake TFF inahitaji Kuungwa Mkono zaidi kwa Hatua Madhubuti
inazochukua za Kujisafisha na Kusonga Mbele.
Katika VITA hii ya
Kupambana na Udhalimu kwenye Mpira wetu Hatutarudi Nyuma, Tutapambana bila hofu
wala woga almuradi Hakuna dhulma wala Uonevu wala Upendeleo kwa yeyote. Na
Nitoe wito kama kuna Kiongozi au Mdau yoyote anayejua ana Pesa za TFF kinyume
cha Utaratibu Natoa WITO Ajisalimishe Mwenyewe.
Ahsanteni kwa
kunisikiliza naamini mtaniunga mkono ili kuusogeza mbele Mpira wa Tanzania.
Mwisho niwakumbushe TFF
inaendelea na maandaalizi ya Matayarisho wa AFCON U 17,2019 .Timu ya ukaguzi ya
CAF itakuja mwezi wa Tano, tumekuwa tunalifanyia kazi kwa ukaribu na serikali kuhakikisha changamoto za viwanja
vitavyochezea mashindano pamoja na viwanja vya mazoezi vinakuwa tayari kwa
wakati.Tutaendelea kulitolea ufafanuzi kila wakati.
0 comments:
Post a Comment