Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Mohammed Kiganja akitoa maelekezo kwa kamati ya ngumi za kulipwa wakati wa kikao chao na mapromota wa ngumi hizo. |
Katibu mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa Mohamed Kiganja ameitaka kamati ya muda ya kusimamia ngumi za kulipwa Nchini, kutengeneza utaratibu mzuri kwa kuzingatia kuwa mabondia wote wanaotoka na kuingia nchini wanavibali kwa kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye sheria ya BMT.
Katibu Kiganja ameyasema hayo katika kikao cha kamati hiyo na wakuzaji wa mchezo wa Ngumi kilichofanyika katika moja ya kumbi za uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, ikiwa ni muendelezo wa Kamati hiyo kuendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau wa mchezo wa ngumi nchini.
“Tengenezeni utaratibu mzuri kwa kuzingatia kuwa mabondia wote wanaotoka na kuingia nchini wanakuwa na vibali kwa kuzingatia sheria ya baraza,” Alisema Kiganja.
Aidha Katibu Kiganja alitoa wito kwa kamati hiyo kuandaa utaratibu wa kuwa na fomu zitakazotumiwa na wadau wa ngumi za kulipwa kufanya malipo na kuombea vibali vya kuandaa mapambano, kulipia ada mbalimbali na kuomba ruhusa kutoka au kuingia nchini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya muda ya kusimamia ngumi za kulipwa Emmanuel Saleh, amesema kwamba popote penye mabadiliko lazima changamoto ziibuke kwa pande mbili zinazokinzana wanaokubali na wanaokataa, lakini lazima tukubaliane na changamoto ili kufikia malengo ya maendeleo ya tasnia ya ngumi za kulipwa Tanzania.
“ Sisi wote ni wanafamilia wa ngumi, lazima tukubaliane na hali yoyote ile ili tufike pale tunapotaka na kuhakikisha kuwa tunaleta maendeleo katika tasnia ya ngumi za kulipwa,” Alisema Saleh.
0 comments:
Post a Comment