Mshambuliaji wa Simba Emmanuel Anord Okwi akishangilia moja ya magoli yake na mchezaji mwenzake Ramadhani Shiza Kichuya |
Mshambuliaji machachari kutoka nchini Uganda Emmanuel Arnord Okwi aliyeingia katika kipindi cha pili akitokea benchi na kufunga mabao mawili wakati klabu yake ya wekundu wa msimbazi Simba SC ikishinda 4-0 dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Simba SC ifikishe pointi 29 kileleni, baada ya kucheza mechi 13, ikiwazidi pointi saba mabingwa watetezi na watani wao klabu ya Yanga SC na pointi mbili Azam FC wenye 27 katika nafasi ya pili, wakati Mtibwa Sugar sasa ni ya tatu kwa pointi zake 24 baada ya timu zote kucheza mechi 13.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara, aliyesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Gasper Ketto wa Arusha hadi mapumziko Simba SC walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0.
Kiungo Shiza Ramadhani Kichuya ndiye alianza kuifungia Simba SC goli dakika ya tatu akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo mkongwe Mwinyi Kazimoto, kufuatia John Raphael Bocco kuangushwa nje kidogo ya boksi.
Beki Mghana, Asante Kwasi akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 25 akimvisha kanzu kipa Peter Manyika aliyetoka langoni bila hesabu nzuri baada ya pasi ndefu ya kiungo Said Ndemla aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kazimoto.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya Singida United wanaofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na kuwaruhusu Simba kutawala zaidi mchezo huo.
Kipindi cha pili, mashabiki wa Simba SC wakaripuka kwa shangwe baada ya kumuona kocha wao mpya, Mfaransa Pierre Lechantre aliyeongozana na msaidizi wake, kocha wa viungo, Mmorocco Mohammed Aymen Hbibi jukwaa kuu.
Okwi akitokea benchi dakika ya 65 kuchukua nafasi ya kiungo Muzamil Yassin na akafunga mabao mawili ndani ya dakika saba.
0 comments:
Post a Comment