![]() |
Mkurugenzi wa Michezo,Yusuph Omary |
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema kwamba inaunga
mkono juhudi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika
programu za maendeleo ya vijana, hususani nia yake ya dhati kushiriki
michuano ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan mwaka 2020.
Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari ndiye aliyesema hayo mara baada
ya kusikia program za TFF kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Makamu Rais wa Kamati ya Olimpiki
Tanzania (TOC), Henry Tandau katika hafla ya uzinduzi wa kampeni
maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki.
“Nimesikia program mbalimbali za TFF, naona zinakuja wakati mwafaka.
Nimewapongeze kwa mipango yenu mizuri kwa sababu inaleta matumaini.
Jambo kubwa ambalo linanisukuma na kuwapongeza ni kuwa na program ya
vijana, hatuwezi kufanikiwa kama hatutakuwa na program ya vijana.
“Serikali inatambua haya yote mnayofanya. Na ili kuboresha, Serikali
imetenga shule 55 ambazo zitakuwa ni maalumu kwa ajili ya vijana, lengo
ni kupata vipaji bora ambavyo vitakuwa vikiendelezwa, huku wakiwa
wanapata elimu.
“Watanzania wana kiu kubwa ya mafanikio, lakini tunafikaje katika
katika safari hii tunayoianza leo? Tutafika tu, iwapo kutakuwa na
ushirikiano licha ya kutoangalia aina ya usafiri ambao tutatumia,”
alisema Singo huku wadau wa mpira wa miguu wakimsikiliza kwa makini.
Aliendelea, “Nasikia mmeunda Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu
hususani vijana. Ni jambo zuri, lakini rai yangu ni kwamba watakaunda
kamati ya mfuko huo wawe watu respected ili wananchi waipende na ikiwa
hivyo itafanikiwa. Sisi Serikali tutafanya kazi bega kwa bega na kamati
hiyo. Jambo kubwa, ni kwamba lazima tukutane mara kwa mara.”
Kabla ya Mkurugenzi Singo kuzungumza, Makamu Rais wa TOC, Ndugu
Tandau, alipongeza pia harakati za kuanza mapema akisema: “Shukrani TFF
kwa kuthamini TOC. Ni vizuri tumeanza mapema. Michuano ya Olimipiki ni
mikubwa na inahitaji timu zenye viwango vya juu kufanikiwa kufuzu.”
Alieleza hadhara iliyohudhuria hafla hiyo, kuwa TOC inakuwa na
Mawasiliano ya maandalizi Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki inayoitwa
‘Olympic Solidarity Program’ ambayo hutoa sehemu ya fungu ya maandalizi
na kwamba TFF haina budi kuwasilisha program yake kwa ajili ya kuingia
kwenye bajeti ambayo inaitwa ‘Team Support Grant’.
“Sasa tuwe kitu kimoja toka huu mwanzo na mambo yaende kwa uwazo na kupeana taarifa kila wakati,” alisema Tandau.
Awali kabla ya viongozi hao kuzungumza, Rais wa TFF, Jamal Malinzi
alisema kinachofanywa sasa na Shirikisho si kutafuta miujiza kwenye
matokeo badala yake ni kujenga timu (Maandalizi) kwa dhana kwamba “Timu
za Taifa haziokotwi kama embe dodo.”
“Mhe. Mkurugenzi, kujenga timu hizi ni gharama kubwa. Hata matunda
ambayo tunasubiri moshi mweupe ya timu ya vijana, hayakutokea hivi hivi
ni maandalizi. Si ajabu kabla ya mwisho wa wiki hii tukaona moshi
mweupe,” alisema Malinzi.
Alisema ili vijana wa Tanzania waweze kufanya vema, hakuna budi wadau
wakiwamo Serikali, Kampuni, Mashirika ya umma na watu binafasi kusapoti
mbio hizo za kwenda Tokyo, Japan pamoja na timu nyingine za taifa.
“Program nzima ni gharama kubwa,”
Kadhalika, ili kutekeleza program hiyo, Rais Malinzi alizungumzia
utulivu katika kufanya kazi kwa sasa kwa kuwa historia inaonesha kuwa
kumekuwa na nia ovu ya baadhi ya wadau kutaka kutibua mambo mazuri
yanayofanywa na uongozi wa mpira wa miguu.
“Naomba tuelekeze mafanikio yetu kwa kushirikiana na kuutendea haki
mpira wa miguu kwa kushirikiana kwa sababu soka ni furaha na ili
kufanikiwa linahitaji juhudi za pamoja,” alisema Malinzi.
..………………………………………………………………………… ........................
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 comments:
Post a Comment