Mambo yanazidi kwenda moto kwa mshambuliaji Thomas Ulimwengu baada ya kupata ofa nyingine ya dola milioni 1 (zaidi ya Sh bilioni 2.2).
Klabu kubwa zaidi barani Afrika ya Al Ahly ya Misri ndiyo imetoa ofa hiyo kubwa ikimtaka Ulimwengu ambaye sasa ni mchezaji huru ajiunge nayo.
Said El Amry, mmoja wa mawakala wanaofanya kazi na Al Ahly katika suala la kusaka wachezaji ameliambia Championi kuwa Ahly wako tayari kumwaga kitita hicho katika mafungu mawili.
“Wanataka mkataba wa miaka minne, akishasaini watalipa asilimia sabini na tano ya fedha hizo. Halafu mwaka unaofuata mwishoni, watamalizia asilimia zilizobaki.
“Tumefanya mazungumzo na wakala wake, lakini hatujajua kama amekubali. Inaonekana ni kama hamsini kwa hamsini. Maana ametuambia bado kuna timu za Ulaya pia zinamhitaji,” alisema.
Juhudi za kumpata meneja wake Ulimwengu zilifanyika kwa siku mbili hadi juzi alipozungumza na gazeti hili kusema wao wanataka kwanza kabisa aende Ulaya.
“Kweli, tunajua Al Ahly inamhitaji Ulimwengu na kila kitu kipo wazi. Lengo namba moja ni kwamba aende Ulaya na huo ndiyo mpango.
“Kuna timu za Ulaya zinamtaka na mazungumzo yameanza. Sisi tumelenga zaidi Ulaya. Kuna Al Ahly, timu nyingine za Misri, pia ziko za Afrika Kusini. Acha tuangalie Ulaya,” alisema Jamal Kisongo.
Tayari KRC Genk ya Ubelgiji ambayo anacheza Mbwana Samatta imeonyesha nia ya kumtaka Ulimwengu ambaye aliamua kutosaini mkataba na TP Mazembe.
SOURCE: CHAMPIONI
0 comments:
Post a Comment