Baada ya kukosa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Ethiopia,
timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepata mwaliko wa kucheza na
Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika
jijini Harare, Novemba 13, mwaka huu.
Kama ilivyotokea kwa Ethiopia kuomba nafasi hiyo kwa Tanzania, pia
Zimbabwe imefanya hivyo na mara moja Tanzania imethibitisha kucheza
mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa wenye kutoa tathmini ubora ili
kuingia kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA).
Kuikosa Ethiopia ambayo ilitoa taarifa baadaye kuwa isingeweza
kuihodhi Taifa Stars kwa sababu ya hali mbaya ya hewa kwa kipindi cha
Oktoba mwanzoni, kulisababisha Tanzania iliyokuwa imejiandaa kucheza
mechi hiyo kushushwa kwa kiwango kikubwa nafasi ya ubora wa viwango vya
FIFA kutoka ya 132 hadi zaidi ya 144. Zimbambwe kwa sasa ni ya 110 na
Ethiopia ni ya 126.
Tayari Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amepewa
majukumu ya kuanza maandalizi na wakati wowote wiki hii atatangaza
kikosi ambacho kitawavaa vijana hao wa Mheshimiwa Rais Robert Mugabe wa
Zimbabwe.
“Ni kipimo kizuri, ni timu nzuri kucheza nayo,” alisema Mkwasa alipozungumza na Mtandao wa TFF ambao ni www.tff.or.tz.
Taifa Stars ambayo kwa sasa haina mashindano au kujiandaa na
mashindano yoyote baada ya kutolewa nafasi ya kuwania Kombe la Mataifa
ya Afrika, inajipanga huku ikisubiria ratiba mpya za Baraza la Mpira wa
Miguu Afrika Mashariki (CECAFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
0 comments:
Post a Comment