Na Samuel Samuel
Safu ya ulinzi ya African Lyon leo itakuwa na kibarua cha
aina yake kuizuia safu ya ushambuliaji ya Simba SC yenye uchu mkubwa wa
kuipatia ubingwa timu hiyo msimu huu bila kupoteza mchezo hata mmoja.
Shiza Kichuya kiungo mshambuliaji wa pembeni wa Simba SC
anaongoza katika orodha ya wafungaji wa ligi kuu kwa mzunguko huu wa
kwanza wa ligi, akiwa na goli 9 kibindoni. Huyu ndie anatazamiwa kuwa
mwiba mkali kwa wageni wa ligi African Lyon akiwa na uwezo wa kufunga,
kuchezesha wenzake pia kusaidia kukaba.
Ukiangalia orodha ya wafungaji bora 10 wa ligi kuu ,
Kichuya ndio mchezaji pekee anaeingia katika orodha hiyo kutokea Simba
SC tofauti na mpinzani wao African Lyon ambaye hana hata mchezaji mmoja.
Kocha wa African Lyon mreno Bernardo Tavares anaetumia
mfumo wa 4-4-2 anaposhambulia na 4-5-1 timu inapojilinda, ana kazi ya
ziada kukiongoza kikosi chake kuibuka na ushindi dhidi ya Simba SC chini
ya Joseph Omog ambaye ameweza kukiongoza kikosi chake katika michezo 13
kushinda michezo 11 na kutoka sare michezo 2.
Hood Mayanja ndio mchezaji tegemeo katika kikosi cha
African Lyon akiwa na goli 3 mpaka sasa ambaye mwalimu Bernardo mara
kadhaa amekuwa akisuka kikosi chake kumzunguka yeye mwenye uwezo mzuri
kuisumbua ngome ya wapinzani kwa mashuti yake na kuicheza mipira
iliyokufa ingawa ubovu wa safu ya kiungo ya African Lyon na eneo la
ulinzi , umeifanya timu hiyo kupoteza michezo mingi na kujikuta
wakiangukia nafasi ya 11 katika ligi baada ya kucheza michezo 14
wakishinda michezo 3 tu , sare 5 na kufungwa michezo 6.
African Lyon wana uwezo wa kuizuia Simba SC wakijipanga
vyema eneo la kiungo na safu yao ya ulinzi. Kocha mkuu wa Simba SC ana
utofauti mkubwa na waalimu wengi ndani ya ligi kuu ambao wanazitengeneza
timu zao kuwazunguka " key players" kusaka ushindi.
Omog ameisuka Simba SC katika mfumo ambao mchezaji yoyote aliyeko katika safu ya ushambuliaji ana uwezo wa kufunga .
Jonasi Mkude kiungo wa chini wa Simba SC ndio roho ya timu
hiyo katika kujilinda na kushambulia. Yeye ndie anaamua goli lipatikane
kupitia upande upi na anasimama imara kuwalinda walinzi wake wa kati.
Lyon wanahitajika kuipasua Simba SC kuanzia eneo la kiungo
alipo Mkude , Mzamiru na kiungo mchezeshaji Mwinyi Kazimoto. Wakiweza
kuikataa Simba kujenga mashambulizi yake tokea kati basi wanaweza
kuifunga timu hiyo au kutoa sare.
Unapocheza na timu kubwa inayokuzidi sana kimbinu na
kiufundi lazima ujipange vyema kwenye hesabu zako hususani katika ulinzi
na kushambulia.
Mbeya City walifanikiwa kuilaza Yanga SC kwa goli 2-1 kwa
kuchukua tahadhari mapema ambayo pia Lyon wakiitumia wanaweza kuwazuia
Simba SC .
Cha kwanza ni kujiandaa vyema kisaikolojia katika kupambana
muda wote kusaka ushindi na kukataa hali ya unyonge. Hili huleta makini
katika kusimamia mfumo husika wa mwalimu katika kujilinda na
kushambulia.
Pili ni kupata mbinu rafiki za kuwatoa mchezoni wapinzani
wenu na kuhakikisha wanaingia katika mtego wa paniki ili kuua uelewano
wa kimbinu uwanjani.
Mwisho matumizi sahihi ya kila nafasi mnayoipata langoni
mwa mpinzani wenu hususani mashambulizi ya kushitukiza na mipira
iliyokufa.
Simba SC ni wazuri sana kwa kushambulia wakijenga pasi fupi
fupi za kasi tokea kati lakini kwa timu makini katika kushambulia
hususani kwa mipira mirefu ya krosi tokea pembeni , unaweza ifunga timu
hii kutokana na uwezo mdogo wa kipa wao Vicent Agban kucheza krosi na
kufanya timing katika kutoka kwenye one against one . Uchache wa magoli 3
mpaka sasa aliyofungwa , unabebwa vyema na uimara wa beki yake.
Tukiangalia upande wa Simba SC yenye uchu mkubwa kutwaa
ubingwa msimu huu wa 2016-17 ni ngumu kidogo kupoteza mchezo huo
ukilinganisha uwezo wao kimbinu na kiufundi dhidi ya African Lyon.
Wameshinda mechi 11 na wakitoka sare mara mbili tu ! hii
peke yake inawajenga vyema kisaikolojia kuusaka ushindi wa 12 katika
mchezo wa kesho.
Mfumo wa ushambuliaji wa timu hiyo unaojengwa na viungo
makini kama Jonasi Mkude , Mzamiru , Mwinyi Kazimoto na kiungo
mshambuliaji anaekuja kwa kasi hivi sasa Mohamedi Ibrahimu anaesimama
kama Play maker na mshambuliaji namba mbili , unaifanya safu ya
ushambuliaji ya Simba SC kuwa tishio .
Lyon wana matatizo katika kujipanga katika safu yao ya
ulinzi hii imewafanya kupoteza mechi 6 na magoli mengi ya kufungwa,
Simba ni wazuri kutumia nafasi na kuwavuruga wapinzani kwa mashambulizi
yao ya kasi , hii inanifanya nione kesho Lyon kama hawatakuwa makini
watawapa fursa Simba kucheka na nyavu.
Bukungu upande wa kulia na Zimbwe Jr kushoto ni hazina
kubwa ya Simba SC katika mfumo wao wa 4-4-2 ambao unaruhusu walinzi wa
pembeni kupanda juu kusaidia mashambulizi . Lyon wana kazi ya ziada
kuzuia mshambulizi ya upande yenye kasi toka kwa wachezaji hawa.
0 comments:
Post a Comment