Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wenye umri wa chini ya
miaka 17 – Serengeti Boys, imeanza rasmi kambi ya wiki moja kabla ya
kwenda Korea Kusini ambako itashiriki michuano maalumu ya kimataifa
iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Korea Kusini.
Timu hiyo itapiga kambi kwa wiki moja kwenye Hosteli za TFF zilizoko
Uwanja wa Kumbukumbiu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Tayari
vijana wameripoti kwenye hosteli hizo tangu jana Oktoba 31, 2016.
Ikiwa Korea, itashiriki michuano hiyo kwa siku takribani 10 kabla ya
kurejea nchini ambako itapangiwa programu nyingine ikiwa ni kucheza na
nyota 40 walioteuliwa na Airtel baada ya michuano ya Kampuni hiyo ya
simu iliyofanyika mwaka huu kwenye kona mbalimbali nchini kabla ya
fainali zake kufanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Serengeti Boys imepata nafasi hiyo
kutokana na umahiri wake wa kucheza soka la ushindani kwani kwa kipindi
cha mwaka mmoja tu, imeweza kucheza michezo 16 ya kimataifa ambako
imekuwa ikifanya vema katika mechi 15 kabla ya 16 iliyopoteza dhidi ya
Congo-Brazaville katika michuano ya kuwania nafasi ya kucheza Kombe la
Mataifa ya Afrika.
0 comments:
Post a Comment