KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amesema kikosi chake kilikuwa bora zaidi ya Yanga kwenye mchezo wa jana, huku akidai jambo pekee lilikosekana ni bahati ya kufunga mabao.
Mchezo huo ulishuhudiwa ukiisha kwa sare ya bila kufungana, ambao uliifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 12 ikiwa nafasi ya saba kwenye msimamo.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Hernandez alisema kikosi chake kilifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi lakini tatizo pekee lililonekana ni namna ya kuzitumia nafasi hizo.
“Tulikuwa na mchezo mzuri sana, tuliwazidi kila kitu Yanga, lakini tulikuwa na bahati mbaya ya kufunga mabao, tutaendelea kufanya kazi kila siku kwa wakati huu kabla ya kulitatua tatizo hilo Novemba kwa kukiongezea nguvu kikosi,” alisema.
Katika hatua nyingine, alisema tatizo la sehemu ya ulinzi tayari ameshalipatia dawa na hii ni kutokana na kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji waliocheza nafasi hizo.
“Katika mechi za nyuma kulikuwa na tatizo kubwa kwenye eneo la ulinzi, na hii imesababishwa na kutoka na kuingia kikosini kwa wachezaji wa nafasi hizo kutokana na majeraha wanayopata, lakini jana wachezaji wote wazoefu wa nafasi hizo walikuwa fiti na hakukuwa na makosa,” alisema.
Wachezaji waliocheza eneo la ulinzi jana ni mabeki wa kati Daniel Amoah na Aggrey Morris huku Erasto Nyoni na Himid Mao wakicheza kama mabeki wa pembani kushoto na kulia.
Azam FC jioni hii itaanza maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaofanyika keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
0 comments:
Post a Comment