Swansea City wamemfukuza meneja wao Francesco Guidolin ikiwa ni siku yake ya kutimiza miaka 61 ya kuzaliwa na kumteua kocha wa zamani wa Marekani Bob Bradley kurithi mikoba hiyo
Guidolin amekuwa kocha wa Swansea tangu mwezi Januari na amefukuzwa baada ya timu hiyo kupata alama nne tu ndani ya michezo saba ya Premier League msimu huu na kufanya kuwa meneja wa kwanza kufukuzwa kwenye ligi ya England.
Mchezo wa mwisho wa meneja huyo wa Kiitaliano ulikuwa ni ule dhidi ya Liverpool ambapo walipoteza kwa magoli 2-1 baada ya kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1.
Bradley, 58, anaacha majukumu yake kwenye klabu ya Ligue 2 ya Le Havre na kuanza rasmi kibarua chake katika klabu ya Swansea, huku akitarajiwa kuanza kibarua chake cha kwanza dhidi ya Arsenal Oktoba 15 baada ya wiki ya kupisha michezo ya timu za taifa
Ameshawahi kufundisha soka kwenye timu ya Stabaek ya Norway na Misri ambapo alidumu kwa miaka miwili, lakini hasa anakumbukwa wakati alipokuwa kocha wa timu ya taifa ya Marekani kati ya mwaka 2006 na 2011, na kuliongoza taifa hilo kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 na kuishia hatua ya 16 bora.
Le Havre, ambao wamemteua Oswald Tanchot kurithi mikoba ya Bradley, wametoa shukrani zao za dhati kwa Mmarekani huyo baada ya kuthibitisha taarifa za kuondoka kwake
"Swansea City wanathibitisha kwamba klabu imeamua kuachana na meneaj Francesco Guidolin," taarifa kutoka tovuti ya Swansea imeeleza.
"Nafasi yake itazibwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya USA Bob Bradley baada ya kufikia makubaliano na klabu yake ya Le Havre ya Ufaransa punde tu baada ya mcnezo dhidi ya Sochaux ."
0 comments:
Post a Comment