Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga
faini ya sh. 5,000,000 (milioni tano) klabu ya Simba, kuiagiza ilipe
gharama za uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki wake katika mechi
ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Oktoba
Mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pia Kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika jana (Oktoba 4,
2016), imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya
aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza
mechi bila washabiki. Adhabu dhidi ya Simba imetolewa kwa mujibu wa
Kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu.
Vilevile kwa kuzingatia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu, Kamati imefuta
adhabu ya kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi wa mechi hiyo kwa Jonas
Mkude wa timu ya Simba baada ya kuthibitika bila mashaka kuwa nahodha
huyo hakustahili kadi hiyo.
Mbali ya ripoti ya Kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo
iliyoonyeshwa 'live', Kamati inaendelea na uchunguzi wa jambo lingine
kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya, na wasaidizi
wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutangaza uamuzi wake.
0 comments:
Post a Comment