Wakata Miwa wa Kagera Sugar kwa mara nyingine tena leo wameruhusu kipigo cha pili mfululizo katika Uwanja wao wa Kaitaba baada ya kufungwa na Azam FC magoli 3-2 katika muendelezo wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika mchezo huo timu zote zilianza kushambuliana kwa kiviziana na kusababisha kuchelewa kupata magoli katika kipindi hicho cha kwanza.
Hatimaye dakika ya 32 Kagera walipata bao la kuongoza kupitia kwa mshambulizi wao mkongwe Temi Felix aliyeunganisha mpira kutoka winga ya kulia na kukwamisha mpira wavuni huku kipa wa Azam Aishi Manula akikosa cha kufanya.
Goli hilo halikudumu sana kwani kiungo mshambuliaji wa Azam FC Mudathir Yahya alisawazisha bao dakika ya 40 baada ya kupata pasi mujarab ya kichwa kutoka kwa nahodha wao John Bocco.
Kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa zimetoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kuanza kwa kasi na kutafuta bao la kuongoza na walikuwa ni Kagera Sugar tena ambao walipata bao la pili na la kuongoza kupitia kwa Temi Felix kwa mkwaju wa penati dakika ya 68.
Azam walijitahidi kwa kadri ya uwezo wao na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 80 kupitia kwa Frank Domayo ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Jean Baptiste Mugiraneza kufuatia kupiga shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 na kuamsha ndoto za Azam kutafuta bao la ushindi.
Azam kwa mara nyingine tena walipata bao la tatu na la ushindi dakika ya 86 kupitia kwa nahodha wao John Bocco kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi maridhawa kutoka winga ya kulia na kuanza kufufua ndoto za wanalambalamba hao kuwania ubingwa wa VPL msimu huu.
Kwa matokeo hayo sasa Azam wamefikisha alama19 na kushika nafasi ya 4 baada ya kuwashusha wote kwa pamoja Mtibwa Sugar (pointi 17) na Kagera Sugar (pointi 18).
0 comments:
Post a Comment