KIUNGO mkabaji wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Jean Mugiraneza ‘Migi’, bao alilofunga dhidi ya Ruvu Shooting juzi linafungua ukurasa mpya kwake wa kupachika mabao zaidi katika mechi zinazokuja za timu hiyo.
Hilo ni bao la kwanza la kiungo huyo kuwahi kuifungia Azam FC tokea alipojiunga na timu hiyo Julai mwaka jana, alilofunga kwa kichwa kufuatia kona ya Khamis Mcha, ambaye ndiye aliyefunga bao pili kwa mabingwa hao katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ulioisha kwa sare ya mabao 2-2.
Migi aliuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa ana furaha kubwa sana mara baada ya kufanikiwa kufunga bao hilo huku akidai limefungua njia ya mabao mengine yake msimu huu.
“Hilo ni goli lililonifurahisha sana kwani ni la kwanza tokea nifike kwa Azam FC, nasema kama limefungua nji ya mabao yangu msimu huu, Inshaallah mechi zinazofuata na zingine nitahakikisha kwamba naendelea kufunga mabao,” alisema.
Changamoto ya ligi
Nyota huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ ambaye hupendelea kukaa na familia yake, hakuacha kuelezea ugumu uliopo hivi sasa kwenye ligi hiyo, akidai kuwa unatokana na kila timu kujiandaa vema.
“Hakuna timu ndogo hivi sasa, hata ile watu wanayosema ni timu ndogo ikija uwanjani unaona imebadilika, pia timu zote zinapokuja kucheza na Azam FC ninaona zinakuwa timu nyingine kabisa zikicheza kwa hali ya juu na kujituma zaidi,” alisema.
Alisema kuwa licha ya Azam FC kuteleza kwenye michezo iliypopita, bado wataendelea kupambana katika mechi zijazo na kurekebisha hali iliyopo ili kutimiza malengo yao ya kuibuka na ubingwa msimu huu walioukosa msimu uliopita.
Akumbushia alivyokuwa ‘Top Scorer’ Rwanda
Migi anashikilia rekodi ya aina yake nchini Rwanda baada ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu nchini humo mwaka 2014 wakati akiichezea APR, akitupia wavuni mabao 14 huku akiwa kama kiungo mkabaji.
“Kwa APR nilikuwa nafaunga mabao mengi, tena sana sana goli nyingi zilikuwa ni za vichwa na mwaka 2014 mimi nilikuwa mfungaji bora kwa Rwanda niliongoza kwa kufunga mabao 14 nikiwa kama kiungo mkabaji.
“Nilifunga sana kutokana na mfumo wa kocha wa kule, nilikuwa nacheza nikiwa huru, tulikuwa tunacheza viungo wakabaji wawili lakini san asana mimi nilikuwa huru uwanjani, kocha aliniacha huru baada ya kugundua nina kipaji cha kufunga mabao hasa mengi ya vichwa na alikuwa akiniruhusu tukiwa na mpira,” alisema kiungo huyo mwembamba na mrefu.
Aliongeza kuwa: “Nilifunga goli nyingi sana hasa kwenye kona, mipira ya adhabu ndogo kwani nilikuwa napanda, nilikuwa na uwezo wa kupanda na kwenda kutafuta goli, wakati timu inashambulia nilikuwa na uwezo wa kwenda kuwasaidia na ndio maana naweza kusema niliweza kufanikiwa kufunga mabao mengi tofauti na hapa Azam FC.”
Alisema mazingira ya mpira yanabadilika kutokana na kila kocha kuwa na falsafa zake, aliongeza kuwa: “Mimi ni mfanyakazi bosi wangu akiniambia kazi yangu anataka itendeke hivi basi namfanyia vile, ni jambo muhimu sana hili kwenda na maelekezo ya kocha, mfumo unanitaka niwe karibu sana na mabeki basi lazima nifanye hivyo.”
Azam FC ni timu bora
Azam FC ina kauli mbiu yake ya ‘Timu Bora, Bidhaa Bora’ inayojidhihirisha vema, hiyo imeonekana kuendana sambamba na kauli aliyoitoa Migi baada ya kueleza kuwa tokea aanze kucheza soka hajawahi kucheza soka katika timu bora na nzuri kama timu hiyo.
Migi mpaka sasa amechezea timu tatu tofauti ikiwemo Azam FC, mbili nyingine zikiwa ni Kiyovu SC alipoanzia kucheza soka na APR, aliyoichezea kama nahodha kwa miaka nane kabla ya kujiunga kwa matajiri hao wa Tanzania.
“Yaani kulinganisha na timu nilizopita, Azam FC ndio timu ambayo iko juu sana kimazingira na kila kitu imejipanga vizuri, naweza kusema tokea nianze kucheza mpira hii ndio klabu bora niliyowahi kucheza,” alisema Migi ambaye anavutiwa kuangalia filamu za Bongo Movie, akiziangalia sana kupitia King’amuzi cha Azam TV ambayo ina chaneli maalumu kwa filamu hizo inayoitwa Sinema Zetu (Chaneli namba 103).
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, imebadilika sana msimu huu ikicheza soka la hali ya juu lakini baadhi ya mapungufu kwenye eneo la ushambuliaji na ulinzi kutokana na mabeki wengi kuwa majeruhi limekuwa likiinyima ushindi mnono timu hiyo, lakini benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, linaendelea kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
0 comments:
Post a Comment