Leseni ya mchezaji George Mpole ikionesha akiitwa Gerald Mpole |
Madudu kwenye suala la usajili kwenye soka la hapa nchini hususan kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ndiyo kioo cha Taifa kwenye masuala ya soka yanaendelea kuibuka siku hadi siku.
Mengi yamekuwa yakizungumzwa na kuahidi kufanyiwa kazi huku wachezaji na timu mbalimbali kila mwaka wakiendelea kukiuka taratibu za usajili bila kujali athari zinazoweza kujitokeza baadaye, lakini TFF ambao ndio wasimamizi wakuu wakishindwa kabisa kuchukua hatua za kudhibiti madudu haya ama kwa kutofahamu au makusudi.
Hapa akiwa ametumia jina lake sahihi la George Mpole |
Kuna suala jipya ambalo limeibuka kuhusu mchezaji wa Majimaji ya Songea George Mpole. Mchezaji huyu amesajili majina mawili tofauti katika msimu mmoja wa dirisha la usajili la 2016-17 tena kwenye klabu moja.
Leseni ya kwanza inaonesha kuwa anaitwa George Mpole lakini nyingine ikionesha jina la Gerald Mpole.
Taarifa zinaonesha kwamba, TFF imemfungia mchezaji huyu mwaka mmoja kujihususha na masuala ya soka baada ya kufanya tukio hilo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Mbozi Silla Yalonde Wumbura Mwashiozya, mwaka jana mchezaji huyo alisajiliwa Kimondo kwa mkataba wa miaka mitatu kabla ya kuhamia Majimaji na kubadilisha jina kutoka George Mpole mpaka Gerald Mpole.
"George Mpole amefungiwa mwaka mmoja na Tff kwa udanganyifu wa majina. Mwaka jana alisajiliwa na Kimondo kwa kandarasi ya miaka mitatu na baadaye Majimaji wakamuhitaji akaamua kubadilisha jina na kujiita Gerald Mpole.
Yalonde alienda mbali zaidi na kusema kuwa taarifa nyingi za mchezaji huyo zinaonekana kukinzana kutokana na umri wake kutoendana na maisha yake halisi tangu alipoanza kucheza soka.
Anasema:"Alianza kucheza fdl (Ligi Daraja la Kwanza) mwaka 2011 /2012 na Polisi Iringa now (sasa) kipindi hiko nikichezea Majimaji then akaenda Kurugenzi kwa misimu miwili kabla ya msimu wa 2015/2016 kuja Kimondo."
Amesema kukosekana watu makini wa kumshauri ndiyo chanzo kikubwa cha matatizo yaliyotokea kwa mchezaji huyo. "Katika hili viongozi wa timu waliomsajili wanahusika sana na ndiyo maana Afisa Msajili wa TMS katika timu ya Majimaji kafungiwa miaka mitatu," Yalonde aliongeza.
Yalonde ameendelea kusema kwamba tatizo kubwa la masuala haya ni kutokana na kuwa na mifumo mibovu ya ya kiutawala katika masuala ya michezo ambako ndiyo uti wa mgongo wa kutengeneza miundombinu bora katika michezo hapa nchini.
Amefichua kwamba wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Soka la Vijana wilayani humo alikumbana na changamoto nyingi za udanganyifu wa umri kwa vijana ili wapate kushiri michuano mbalimbali ya vijana hali inayohatarisha mustabali wa soka nchini.
"Mwezi March kabla sijaingia ktk mfumo wa soka (ukatibu) niliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Soka la Vijana Wilaya na ilipokuja issue ya umri nilitofautiana na viongozi wote katika mipango ya kudanganya umri."
"Nikaamua kujiuzulu nilipoingia katika uongozi niliwatangaza vita kwa uwazi kabisa na viongozi wawili wamefungiwa kujihusisha na soka katika wilaya yangu kwa mwaka mmoja-mmoja."
Amesisitiza kuwa chanzo kikubwa cha matatizo haya yote ni kuwa na viongozi wasio na weledi, ambao wanaamini hawawezi kuguswa hata ikitokea wametenda makosa, hali inayopelekea taifa kurudi nyuma kila siku katika masuala ya michezo na kukosa cha kujivunia mbele ya mataifa mengine.
0 comments:
Post a Comment