Simba SC leo wameuzindua Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa shangwe baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wanajeshi wa Ruvu Shooting katika muendelezo wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba walianza mchezo huo kwa kasi, huku wakilikosakosa lango la wapinzani wao kila mara kupitia kwa washambuliaji wao hatari Ibrahim Ajibu na Laudit Mavugo.
Lakini hata hivyo juhudi zao zilizimwa mnamo dakika ya saba baada ya Abulrahman Mussa kufunga goli zuri kufuatia pasi nzuri kutoka kwa Fully Maganga.
Baada ya bao hilo Simba walitulia na hatimaye kufunga bao la kusawazisha kupitia kwa Ibrahim Ajibu mnamo dakika ya 11, kufuatia kuunganisha krosi safi kutoka upande wa kushoto iliyochongwa na Mohammed Hussein 'Tshabalala'.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote zilikuwa zimetoshana nguvu ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi hasa kwa upande wa Simba na ndipo walipofanikiwa kuandika bao la pili dakika ya 48 kupitia kwa mshambuliaji wao nyota kutoka Burundi Laudit Mavugo, ambaye aliunganisha pasi nzuri kutoka kwa Ibrahim Ajibu.
Kiungo wa Ruvu Shooting, Jabir Aziz alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 79 baada ya kumchezea rafu kiungo wa Simba SC, Mzamiru Yassin aliyekuwa akienda kuliona lango la Ruvu Shooting.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inafikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, baada ya hapo awali kushinda 3-1 dhidi ya Ndanda FC kabla ya kulazimishwa sare ya 0-0 na Wanajeshi wa JKT Ruvu.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Malika Ndeule, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Jamal Mnyate dk80, Said Ndemla/Mzamiru Yassin dk71, Laudit Mavugo/Frederick Blagnon dk64, Ibrahim Hajib na Mwinyi Kazimoto.
Ruvu Shooting: Abdallah Rashid, Damas Makwaya, Mau Bofu, Frank Msese, Shaibu Nayopa, Jabir Aziz, Abulrahman Mussa/Baraka Mtuwi dk51, Shaaban Kisiga, Said Dilunga, Fully Maganga na Claide Wigengea
0 comments:
Post a Comment