Wekundu wa Msimbazi Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuwandatika Wanalizombe Majimaji ya Songea mabao 4-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakicheza soka safi na la kuvutia Simba walionekana na kila dalili za kuibuka na ushindi mnono kwenye mchezo wa leo kufuatia kusukuma mashambulizi ya mara ya kwa mara langoni mwa Majimaji.
Jamal Simba Mnyate ndiye liyefungua milango ya mabao kwa Simba leo dakika ya 4 baada ya kufunga goli kufuatia uzembe wa kipa Amani Simba kuutema mpira uliopigwa na Ibrahim Ajibu.
Bao hilo lilidumu mpaka mapumziko wakati timu hizo zilipokwenda kupata mawaidha kutoka kwa walimu wao.
Dakika ya 21 Simba ilipata pigo baada ya mshambuliaji wake tegemeo, Ibrahm Ajibu kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikichukuliwa na kiungo Said Ndemla.
Kipindi cha pili Simba walianza kama nyuki na kupata bao la pili dakika ya 67 kupitia kwa nyota wake Shizza Kichuya kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Majimaji Lulanga Mapunda kuunawa mpira huo.
Jamal Mnyate aliifumgia Simba bao la tatu na la pili kwa upande wake dakika ya 74 kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Mohammed Ibrahim aliyewahadaa mabeki wa Majimaji na kupiga krosi nzuri iliyotua mguuni kwa Mnyate.
Shiza Kichuya alimaliza karamu ya magoli kwa Simba huku naye likiwa goli lake la pili katika mchezo dakika ya 81 baada kufunga goli zuri kufuatia pasi nzuri ndefu iliyopigwa na kiungo mkabaji na nahodha wa timu hiyo Jonas Mkude.
Simba sasa wanafikisha alama 16 baada ya kucheza mechi sita, wakishinda mechi tano na kutoka sare mara moja.
Mpaka sasa Majimaji hawajashinda mchezo wowote huku wakiwa wamepoteza michezo yote.
0 comments:
Post a Comment