Manchester United jana walikuwa na kibarua kingine Europa League dhidi ya Zorya Luhansk na kushinda bao 1-0, mchezo ambao kocha wa United Jose Mourinho alisema ni lazima ushindi upatikane.
Katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Old Trafford, United walionekana kukosa ubunifu hasa kwa baadhi ya wachezaji wao akiwemo Marouane Fellaini.
Paul Pogba ni mchezaji ghali zaidi duniani kwa sasa ambaye United wamemnunua dirisha la usajili la kiangazi, lakini bado wanashindwa kujua ni wapi hasa mahali sahihi wamchezeshe staa ili aweze kung'aa kama alivyokuwa akifanya Juventus. Kwenye michezo kadhaa aliyocheza pamoja na Fellaini, Pogba alionekana kucheza tofauti na wakati ambapo Fellaini hayupo. Vilevile jana kwenye mchezo dhidi ya Zorya hadhithi ilikuwa ileile.
United walikosa kabisa njaa ya kulisakama lango la wapinzani wao. Watu wanajiuliza je, kama angecheza Michael Carrick hali ingekuwa vilevile kama ambavyo alicheza Fellaini? Wakati ambapo ama Carrick au Ander Herrera wamecheza nyuma ya Pogba, United wamekuwa wakionesha utofauti mkubwa sana.
Ili Pogba aweze kucheza izuri vizuri pembeni yake anahitaji mtu ambaye ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi nzuri vilevile mwepesi na mwenye kasi.
Na watu hao kwa United ni Herrera na Carrick. Wakati mwingine ugumu unakuja kwa Mourinho kutokana na aina ya wachezaji anaopendelea kuwatumia.
Mara nyingi Mourinho anapenda kutumia wachezaji wenye miili mikubwa ili kuweza kufanikisha aina ya soka lake linaloendana kwa kiasi kikubwa na matumizi ya nguvu kubwa uwanjani, na ukizungumzia aina hiyo ya mfumo basi Fellaini anaonekana kuwa sahihi.
Lakini kwa aina ya soka la sasa la England, matumizi ya nguvu yanahitajika lakini vilvile matumizi ya akili. Pogba ni mchezaji mwenye vitu hivyo vyote viwili, nguvu pamoja na matumizi ya akili.
Sasa mara nyingi akichezeshwa na Fellaini ambaye anategemea zaidi matumizi ya nguvu anakosa usaidizi hasa katika kupiga pasi nzuri ambazo zinaweza kumfikia na kupeleka madhara kwenye lango la wapinzani.
Suluhisho pekee la Pogba kuweza kung'aa, kuonesha na kuthibitisha thamani ni kumchezesha pamoja na ama Ander Herrera au Michael Carrick, viungo ambao wanaweza kumpa muunganiko mzuri hasa kwenye upigaji mzuri wa pasi pamoja na uwezo wao mkubwa wa kuusoma mchezo.
Pogba bado ana nafasi ya kuonesha kile alichokuwa akikifanya Juventus wakati huo akiwa na kina Arturo Vidal, Andrea Pirlo na wengineo.
0 comments:
Post a Comment