Arsenal watakuwa wenyeji wa FC Basel kesho katika mchezo wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaofanyika kunako Uwanja wa Emirates.
Mchezo huu utakuwa na msisimko wa aina yake kutokana rekodi nzuri ya FC Basel dhidi ya timu za England, vile vile morali ya Arsenal baada ya kuwa na mwenendo mzuri kwenye michezo ya EPL hasa baada ya kuwanyuka mahasimu wao Chelsea mabao 3-0 mwisho mwa wiki iliyopita.
Msisimko zaidi unakuja pale ndugu wawili wa damu Granit Xhaka anayekipiga Arsenal na Taulant Xhaka anayekipiga Basel.
Vijana hawa waliwahi kucheza pamoja kwenye akademi ya Basel wakati wakiwa wadogo kabisa lakini leo hii wanaenda kukutana wakiwa wakubwa na kila mmoja akicheza timu nyingine.
Hii si mara ya kwanza kwa wawili hawa kukutana kwani awali walikutana kwenye Michuano ya Euro 2016 iliyofanyika nchini Ufaransa, Granit akichezea Uswisi na Taulant akichezea Albania
Hivyo, kuelekea mchezo huu, kupitia akaunti yake ya Instagram, Granit Xhaka ameandika ujumbe wenye safari ya kisoka kati ya kaka yake na yeye mwenyewe.
Granit ameandika: FC Concordia Basel ilikuwa ndio timu yetu ya kwanza kujifunza soka. Mwanzoni kabisa, tulichokuwa tunaangalia zaidi ni kucheza na kufunga magoli mengi ipasavyo. Wakati huo nilikuwa nina miaka 5 na kaka yangu akiwa na miaka 6, na sikuwahi kudhani kama tungefika mbali kiasi hiki kama.👌👏. Shukrani nyingi za dhati zimfikie kocha wetu wa kwanza kabisa Andy Eichenberger na makocha wengine wote waliochangia mafanikio yetu mpaka kufikia hatua hii sasa.🙏🙏🙏
0 comments:
Post a Comment