HAKUNA mshambuliaji mwingine yoyote katika soka la Uingereza, aliyewahi kufunga mabao dhidi ya timu moja kwenye mechi nane, zaidi ya nyota wa zamani wa Arsenal na Manchester United, Robin van Persie.
Mholanzi huyo alikuwa akipata sifa kubwa kila alipokuwa akicheza dhidi ya Stoke City na Blackburn Rovers, kwani amefunga jumla ya mabao 24 dhidi yao. Mabao 11 akiwafunga Stoke na akitingisha nyavu za Blackburn mara 13.
Hapa Tanzania kuna mshambuliaji mmoja tu mwenye rekodi ya aina hiyo, ambaye si mwingine ni nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ ukipenda muite ‘The King of Azam FC’ (Hii ni kutokana na makubwa aliyoifanyia timu hiyo hadi sasa).
Nahodha huyo amejijengea heshima kubwa nchini kwa sasa akiwa ni miongoni mwa washambuliaji wanaoogopwa sana na mabeki wengi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Mbali na Bocco kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) alipofunga mabao 19 msimu wa 2011/12, nahodha huyo amejiwekea heshima nyingine kubwa ya kuwa kinara wa kuzifunga mara kwa mara Simba na Yanga.
Bocco aliyefunga mabao mawili muhimu yaliyoipandisha daraja Azam FC mwaka 2008 ilipocheza dhidi ya Majimaji (2-0), mpaka sasa kwa mujibu wa takwimu ameifunga Yanga mabao 12, huku pia akipasia kwenye nyavu za Simba mara 18.
Ukiondoa presha anayoitoa uwanjani kwa mabeki wa timu pinzani, pia presha hiyo imekuwa ikipanda zaidi kwa mashabiki wa timu hizo pale kila mara mshambuliaji huyo anapolikaribia eneo la 18 na hii ni kutokana na uhodari wake wa kuacha maafa kwenye lango lao.
Siku mbili zijazo (Jumamosi ijayo), Bocco anatarajia kuliongoza jeshi la Azam FC kukabiliana na Simba ndani ya Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mechi inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini.
Bocco anaingia kwenye mchezo huo akiwa ndiye kinara wa ufumaniaji nyavu ndani ya Azam FC msimu huu kwa mabao matatu aliyofunga, ambayo pia yanamweka kileleni katika chati hiyo akiwa amelingana mabao na wachezaji wengine watatu wanaofukuzia kiatu hicho.
Ufiti wa Bocco na ubora wa kikosi cha Azam FC msimu huu chini ya makocha kutoka Hispania wakiongozwa na Zeben Hernandez, umezidi kuleta hamasa miongoni mwa mashabiki wa Azam FC ambao wanamatumaini makubwa ya ushindi ikiwemo kikosi hicho kufanya makubwa zaidi hapo baadaye.
Katika pambano la kwanza la msimu uliopita, Bocco aliendeleza moto wake wa kucheka na nyavu dhidi ya wekundu hao baada ya kutikisa nyavu zao mara mbili kwenye sare ya 2-2.
Mpaka sasa kikosi cha Azam FC kina morali kubwa baada ya kujikusanyia pointi 10, zilizotokana na kutoa sare moja na kushinda mechi tatu mfululizo, kati ya pointi hizo sita imevuna kwenye mechi mbili ngumu za ugenini mkoani Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons (1-0) na Mbeya City (2-1).
0 comments:
Post a Comment