Na Mwandishi Wetu, Mbeya
BAADA ya mapumziko ya siku moja yaliyotolewa na kocha Kinnah Phiri kufuatia safari ndefu ya saa nyingi kutoka kanda ya ziwa, kikosi cha Mbeya City fc jana kimeanza mazoezi rasmi kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Azam Fc uliopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa siku ya jumamosi.
Akizungumza na mbeyacityfc.com Afisa habari wa City, Dismas Ten amesema kuwa nyota wote 30 ikiwa ni pamoja na 25 waliokuwa nje ya jiji la Mbeya kwa takribani wiki tatu kwa ajili ya michezo ya mwanzo wa msimu wamejumuika kwenye mazoezi hayo.
“Tumeanza mazoezi leo (Jana), baada ya mapumziko ya siku moja,nyota wetu wote wapo ikiwa ni pamoja na wale ambao hawakusafiri na timu kwenda Mwanza na Shinyanga kwenye michezo mitatu ya Mwanzo wa msimu ambayo tuliikamilisha kwa kushinda miwili na suluhu moja,limekuwa ni jambo jema kwetu kwa sababu morari imeongezeka kikosini na kila mmoja yuko tayari kwa mchezo wa mwishomi mwa juma” alisema.
Akiendelea zaidi Ten alisema kuwa huu ni msimu ambao City imejipanga kuvunja rekodi zote ambazo ilikuwa haijawahi kuzifikia tangu ilipopanda daraja misimu mitatu iliyopita.
“Huu ni msimu ambao kwetu utakuwa na kumbukumbu nzuri kwa sababu tumejipanga kufuta ‘madeni’ yote tuliyokuwa nayo, tangu tumepanda daraja tulikuwa hatukuwahi kuongoza ligi hili sasa limeshakwisha,tunasubiri kuvunja rekodi ya kutokuzifunga Yanga na Azam fc jambo ambalo tuna amini tunalianza wikiendi hii” alitamba.
Wakati huo huo Ten ameweka wazi kuwa mshambuliaji Geofrey Mlawa ni wazi ataukosa mchezo wa jumamosi dhidi ya Azam Fc kufuatia majeraha aliyoapata kwenye mchezo dhidi ya Toto African jijini Mwanza na tayari jopo na madaktari wa City wameshathibitisha jambo hili mbele ya benchi la ufundi.
Mbeya City FC watafanya mazoezi ya Mwisho leo maenei ya Uyole Jijini hapa.
0 comments:
Post a Comment