Tuesday, August 2, 2016

YANGA imefanikiwa kumsainisha mkataba fasta fasta kinda mwenye uwezo wa hali ya juu, anayetabiriwa kuwa bonge la staa na hata kuwafunika nyota wa kigeni waliopo Jangwani kwa sasa.

Mchezaji huyo aliyekuwa akikipiga Yanga B, anafahamika kwa jina la Yusuph Mhilu, akiwa ni kijana mweupe asiye na makeke, lakini akiwa na kipaji cha aina yake katika soka.

BINGWA kwa nyakati tofauti, limewahi kumwona kijana huyo anavyofanya vitu vyake uwanjani kiasi cha kumlinganisha ‘utundu’ wake na nyota wa Brazil anayekipiga Barcelona, Neymar.

Kwa kuwa mchezaji huyo ametokea mikononi mwa beki wa kulia na nahodha wa zamani wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, gazeti hili lilimtafuta mkali huyo kutaka kupata maoni yake juu ya Mhilu, ambapo alikiri kijana huyo atatisha ndani ya klabu hiyo.

“Ana kipaji kikubwa sana na nidhamu yake ipo juu pia. Ni mtu anayependa kujifunza zaidi kila anapopata nafasi, kama akiendelea hivi, nina imani atakuwa na mafanikio makubwa katika safari yake ya soka,” alisema Nsajigwa ambaye pia ameitumikia timu ya Taifa, Taifa Stars  kwa mafanikio makubwa kabla ya kustaafu.

Juu ya uwezo wa kijana huyo uwanjani, Nsajigwa alisema: “Anazimudu namba zote za mbele, anaweza kucheza wingi ya kushoto na kulia na pia ni mzuri anapocheza kama straika wa kati.”

Nsajigwa alipoulizwa iwapo dogo huyo anaweza kuwa na nafasi ndani ya kikosi cha Yanga kulingana na wachezaji waliopo kwa sasa, alijibu: “Hapa uamuzi utabaki kwa mwalimu, ndiye atakayeamua pakumtumia. Lakini kwa kasi yake, nguvu na akili ya kulazimisha mashambulizi, nina imani atafanya makubwa sana kwenye kikosi cha wakubwa.”

Nsajigwa aliipongeza Yanga kwa kumpandisha mchezaji huyo kwani iwapo wangechelewa kufanya hivyo, huenda angerubuniwa na klabu nyingine na kuyeyuka Jangwani alikolelewa chini yake.

Bingwa lilipomtafuta Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, kuelezea uamuzi wake wa kumpandisha mchezaji huyo hadi timu ya wakubwa, simu yake iliita bila kupokewa kama ilivyokuwa kwa meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh.

Lakini mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Yanga ambaye hakutaka jina lake kuwekwa hadharani, alisema: “Ni kweli dogo amepandishwa timu ya wakubwa baada ya kuridhishwa na uwezo wake. Lakini pia, tulipata taarifa kuna timu inamuwinda, hivyo tukasema ni heri tumuwahi.

“Anaonekana ni mchezaji mzuri na umri wake mdogo utamwezesha kucheza mpira kwa muda mrefu na hatutarajii kama atapata shida kupata nafasi kikosi cha kwanza. Kama ataongeza bidii na kufuata maelekezo ya walimu, anaweza kuchukua hata namba za wachezaji wetu wa kigeni nao.”

Imeelezwa kuwa Mhilu alikuwa katika mipago ya Pluijm kwa muda mrefu, hasa baada ya mshambuliaji wake wa kati, Paul Nonga kushindwa kufanya yale yaliyotarajiwa baada ya kusajiliwa akitokea Mwadui FC.

Klabu ambazo zilitajwa kumnyemelea Mhilu ni Simba, Prisons ya Mbeya na JKT Ruvu.

0 comments:

 
https://www.sexmutant.com/ https://www.sexindrag.com/ porn movies sex videos hd porno video