Arsene Wenger tayari ameanza kujitoa kwenye mbio za ubingwa mapema baada ya ya kushuhudia tena timu yake ikitoka suluhu na Leicester City jana. Ni mchezo wa pili huu kwa Arsenal bila ya ushindi na kuwaacha mashabiki wao dhohofu lhali. Washindani wakubwa wa Arsenal msimu huu ni Manchester City, United, Chelsea, Liverpool na hata Tottenham Hotspurs.
Manchester United, Man City na Chelsea tayari zina alama sita kila upande, Liverpool wanazo tatu huku Tottenham wakiwa na alama nne.
Utaona ni namna gani vigogo wenzake wanazidi kuchanja mbuga huku wao wakizidi kurudi nyuma.
Tatizo la Arsenal limekuwa lile lile kila mwaka ila ubishi wa kocha Arsene Wenger wa kuamini timu yake haina matatizo ndiyo kunaigharimu timu hiyo.
Matatizo ya Arsenal yamekuwa ni nafasi ya mshambuliaji wa kati na beki wa kati. Tumeanza kuona kwenye msimu huu mpya, tangu mchezo wa kwanza tumeshuhudia Wenger akimlazimisha Sanchez kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati.
Tuliona hivyo kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Liverpool na jana tena tumeona kwenye mchezo dhidi ya Leicester.
Tumeona akiwaaminisha washabiki kwamba nafasi hiyo Sanchez anaimudu kwa asilimia zote bila matatizo yoyote.
Hivi karibuni baada ya mchezo dhidi ya Liverpool Wenger alisema: “Je, Sanchez ni suluhisho la muda mrefu la Arsenal kwenye nafasi ya ushambuliaji wa kati? nadhani ndiyo, nadhani ni muhimu kumjaribu kwasababu ana sifa zote za kuwa mshambuliaji, ana uwezo wa kuwatoroka mabeki. Akicheza pembeni mwa uwanja hutumia nguvu nyingi kukimbia na kukaba.
“Sasa ningependa kuona nguvu zake zikitumika kwa namna tofauti, akicheza katikati hatatumia nguvu nyingi zaidi ya kucheza na akili za mabeki ukizingatia kwamba ni mfungaji mzuri. Ana ubora ule ule ambao Luis Surez anao. Kiufundi ni mchezaji wa kiwango cha juu sana.”
Ukweli ni kwamba Alexis Sanchez si mshambuliaji wa kati hata ukifanyaje hawezi kuwa mshambuliaji wa kati kutokana na aina yake ya uchezaji.
Sasa baada ya kumfananisha na Luis Suarez, Arsene Wenger jana aliamua kumuanzisha Sanchez kama mshambuliaji wa kati dhidi ya Leicester City. Kwenye mchezo huo Sanchez alionekana kuhangaika kuapmbana na mabeki wa Leicester na kwa hakika alionekana kushindwa kabisa.
Alishindwa namna ya kujiweka katika nafasi nzuri ya kufunga na muda mwingi alikuwa akihangaika kutumia nguvu nyingi na manjonjo mengi kuwahadaa mabeki wa Leicester na hatimaye kushindwa kufanikisha majukumu yanayopaswa kufanya na mtu wa nafasi hiyo.
Huu wote ni ubishi na upofu wa Wenger kujiona ni malaika ambaye anaweza kufanya lisilowezekana kuwezekana.
Haya kituko kingine ni kumtaja mshambuliaji ambaye pengine hana hata hadhi ya kuichezea Arsenal Yaya Sanogo, ambaye licha ya uwezo wake hafifu lakini amekuwa majeruhi kwa muda mrefu sasa na kushindwa kufanya mazoezi na wenzake.
Huyu huyu Sanogo ameshindwa hata kupata nafasi kwenye kikosi cha Ajax ya Uholanzi, ambapo katika kipindi cha miezi sita alichoitumikia tmu hiyo kwa mkopo amecheza dakika 47 tu.
Sasa hivi kweli kama mchezaji anashindwa kupata nafasi Ajax, anawezaji kuwa mchezaji anayetajwa kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwenye timu kubwa kama Arsenal?
Kweli Wenger anazeka vibaya huyu mzee. Nirudi kidogo kwa Sanchez tena, Wenger amesema wakati akiwa Barcelona alikuwa akichezeshwa kama mshambuliaji wa kati na kufanya vyema.
Sidhani kama kuna ukweli juu ya hili, sababu kubwa ya Sanchez kufikia hata hatua ya kuanzia benchi wakati akiwa Barcelona ni kutokana na uwezo wake usioridhisha kwenye nafasi ile hali iliyopelekea kuuzwa Arsena
Je, Barcelona wanaweza kumuuza mchezaji kwenda timu nyingine ilhali wanahitaji mchango wake? Jibu ni hapana.
Unamkumbuka Sanchez wa Udinese? Yule sasa ndiye alikuwa Sanchez ambaye alikuwa akicheza kutokea pembeni. Alijaa ufundi mwingi na kuwa na hatari kubwa kwa wapinzani.
Sanchez hajawahi kuwa bora akicheza kati hata mara moja. Hata kwenye timu yake ya taifa ya Chile hachezi katikati bali hucheza pembeni na huwa na madhara makubwa kuliko kawaida.
Tuachane na Sanchez mwingine anayetegemewa kuwa wa kuipa ubingwa Arsenal eti Danny Welbeck. Ikumbukwe kwamba Welbeck aanuguza majeraha ambayo yatamweka nje mpaka wakati wa Christmas.
Hata kama angekuwepo, Welbeck si mtupiaji mzuri bali ni mpambanaji, ni mtu ambaye hawezi kufikisha hata magoli 18 kwa msimu.
Mwingine Chuba Akpom, mwenye miaka 20 ambaye ni ukweli ulio wazi kwamba ana uwezo mzuri lakini bado si kuaminiwa na kupewa jukumu la kusimama mbele na kuipigania Arsenal kupata ubingwa ilhali wenzao wana Zlatan Ibrahimovic na Sergio Aguero na matusi ya waziwazi.
Jana washabiki wa Leicester City walikuwa wakiwakumbusha kitu washabiki wa Arsenal kuhusu maamuzi ya Jamie Vardy kuikacha Arsenal na kusaini mkataba mpya wa kubaki Leicester. Walikuwa wakiimba: “Vardy ni wa blue, anaichukia Arsenal, akafuatiwa na Riyad Mahrez…ameona kuna ubabaishaji, hakuna harakati zozote za usajili Emirates Stadium majira haya ya joto.”
Licha ya Mahrez kutokuwa kwenye target kubwa ya Wenger, lakini ukimuangalia Vardy alikuwa na umuhimu mkubwa sana endapo angetua Arsenal.
Kuna tatizo kubwa sana Arsenal, ukingalia idadi ya wachezaji ambao Arsenal wamewahi kuhusishwa kuwasajili na baadaye kuwakosa utaona kwamba, safari ya Wenger kuchukua ubingwa bado ndefu sana. Waliwahi kuhusishwa kumsajili Gonzalo Higuain, Alvaro Morata na sasa Alexandre Lacazette, hakuna dalili yoyote ya nyota huyo wa Ufaransa kutua klabuni hapo.
Mshambuliaji pekee asilia kwenye nafasi ya ushambuliaji wa kati ni Olivier Giroud, ambaye jana aliingia dakika za mwisho za kipindi cha pili kufuatia kutoka mapumzikoni baada ya kumalizika kwa Michuano ya Euro mwaka huu.
Giroud mwenye si mshambuliaji anayeweza kukupa ubingwa. Ni mchezaji asiyehangaika uwanjani, hana kasi. Mchezaji ambaye ana udhaifu mwingi kuliko ubora.
Hawezi kuwapa shinda mabeki, uwezo wake wa kupiga chenga ni mdogo, anategemea zaidi mipira ya vichwa, ya kuunganisha na rebound ili kufunga magoli yake.
Arsenal Wenger na ubishi wake namwona kabisa akielekea kuzimu msimu huu. Ubishi wake ndiyo utampa matokeo anayostahili kupata, wakati vigogo wenzake wanazidi kuchanja mbuga. Mwisho wa yote tusubiri mwezi Mei mwakani tuone atawaambia nini tena mashabiki wa Arsenal baada ya kuwaaminisha matumizi ya fedha si kitu pekee kinachoweza kuipata timu ubingwa.
0 comments:
Post a Comment