Taarifa ambazo MPENJA SPORTS imezipata ni kwamba Rais wa Simba Evans Aveva na Wajumbe wa kamati ya Utendaji wa klabu hiyo leo wanatakiwa kuripoti saa tano asubuhi katika Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Inaelezwa wajumbe hao wa kamati ya utendaji nao wanahojiwa kuhusiana na tuhuma za fedha dola 300,000 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Simba katika benki moja, kwenda kwenye akaunti na benki nyingine na kusababisha Rais Aveva kushikiliwa na TAKURURU Agosti 3 ambapo alilala lupango katika kituo cha Polisi, Urafiki, ingawa jana aliachiwa kwa dhamana.
Fedha hizo ni zile za malipo ya mwanasoka Emmanuel Okwi aliyeuzwa dola 319,212 lakini fedha hizo hazikulipwa mapema baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kufanya haraka katika mauzo hali iliyofanya uongozi wa Simba ulioingia madarakani kuanza kuhaha kupambana na Etoile hadi kufikia Fifa ili walipwe.
Mkuu wa Uchunguzi wa Sekta ya Umma ya Takukuru, Leonard Mtalai alisema akaunti hiyo iliyohamishiwa dola 300,000 ni ya Aveva na baada ya hapo, dola 62,000 zilihamishwa kwenda Hong Kong na sasa Takukuru inashirikiana na wenzao wa nchini humo ili kujua kilichonunuliwa kupitia fedha hizo.
Taarifa zaidi zinaeleza fedha hizo dola 62,000 zilitumika kununua nyasi bandia ambazo tayari zimetua nchini kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mazoezi eneo la Bunju na ujenzi umeanza.
Ofisa huyo wa Takukuru, amethibitisha kuhojiwa kwa watu kadhaa pamoja na Aveva na kusema bado wanaendelea na uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment