Mchezo wa mwisho wa Kundi A michuano ya kombe la Shirikisho Afrika kati ya TP Mazembe dhidi ya Yanga umemalizika kwa Yanga kukubali kichapo cha magoli 3-1 ikiwa ugenini na kuendeleza rekodi yake ya kutoshinda michezo yake mitatu ya hatua ya nane bora msimu huu.
Baada ya mchezo huo, Kurugenzi ya Habari ya Yanga ilifanya mahojiano na kocha msaidizi wa klabu hiyo kutaka kujua maoni yake kuhusu ushiriki wa timu yake kwenye michuano hiyo.
" kwanza kabisa tunamshukuru mwenyezi Mungu hapa tulipofikia . Hakika haikuwa rahisi , michuano ilikuwa migumu na tumejifunza mengi . Hata leo kabla ya mechi hii niliwaambia wachezaji wangu hii ni mechi muhimu licha ya kukamilisha ratiba hivyo umakini unahitajika . "Niliwaeleza licha ya kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali lakini tumejifunza vingi kubwa ni suala la nidhamu ya mchezo na nidhamu ya mchezaji husika uwanjani . Timu yetu imeandamwa sana na kadi , mfano Donald Ngoma ni mchezaji tegemeo eneo la ushambuliaji lakini amekosa mechi mbili kwenye hatua hii hali iliyoiathiri timu kwa namna moja au nyingine.
" Yote kwa yote shukrani zetu kwa watanzania waliotupa sapoti muda wote . Watambue mtoto huanza kutambaa kisha hutembea pia msingi imara hujengwa kwa umakini mkubwa . Hivyo huu ndio muda tunaijenga Yanga mpya , Yanga ya ushindani.
"Tunajenga msingi mzuri wa timu kitaifa na kimataifa . Kwa mantiki hiyo tulipofikia si haba , watanzania watuelewe," alimalizia Mwambusi.
Yanga itarejea jijini Dar es Salaam kesho na kuanza rasmi mazoezi siku ya Alhamisi kwaajili ya Ligi Kuu hususan mchezo wa tarehe 28 dhidi ya African Lyon.
0 comments:
Post a Comment