![]() |
Abdul Mingange |
Maafande wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons, 'Wajelajela' wameanza maisha mapya chini ya kocha mpya, Meja Mstaafu Abdul Mingange.
Mingange ameiambia MPENJA SPORTS mchana huu kwamba aliripoti Mbeya Julai 20 mwaka huu na tayari anaendelea na program za mazoezi akirithi mikoba ya Salum Mayanga aliyetimkia Mtibwa Sugar.
Mingange, aliyewahi kuwa kocha wa Ndanda FC na Mbeya City, amesema anafurahishwa na mazingira ya Prisons ambayo ilimaliza msimu uliopita kwa kushika nafasi ya nne ikijikusanyia pointi 51 katika michezo 30 ya ligi kuu soka Tanzania Bara.
"Namshukuru Mungu tunaenda vizuri, lakini tukishaanza ligi ndio tutajua. Naona mazingira ni mazuri, wachezaji wamenipokea vizuri, kiwanja cha mazoezi tunacho, chakula na mahala pakulala pazuri", Ameeleza Mingange.
Wakati huu zimesalia siku tatu kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi Tanzania Bara, Mingange amesema tayari alikuta wachezaji wamesajiliwa kwa kuzingatia ripoti ya Mayanga.
"Mwalimu Mayanga (Salum) alipomaliza (ligi) aliandika ripoti yake, alipendekeza baadhi ya wachezaji na wao (Prisons) walitegemea kwamba wataendelea naye,wamefanya usajili, lakini kaondoka katikati, kwahiyo usajili wake alioufanya namimi naenda nao huo huo. Si wachezaji wabaya aliowasajili". Amesema Mingange.
0 comments:
Post a Comment