Daniel Amouah (wa tatu kutoka kushoto) wakati akisaini Azam FC
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo jioni imeingia mkataba na mabeki wawili, Mghana Daniel Amoah na Mzimbabwe, Bruce Kangwa, kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo jioni imeingia mkataba na mabeki wawili, Mghana Daniel Amoah na Mzimbabwe, Bruce Kangwa, kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Wawili hao kila mmoja amesaini mkataba wa miaka mitatu, Amoah anayecheza beki ya kati ametokea Medeama ya Ghana, huku Kangwa aliyefuzu majaribio ya kujiunga na Azam FC akitokea kwa vinara wa Ligi Kuu Zimbabwe Highlanders.
Amoah, 18, anatua Azam FC ikiwa ni pendekezo la benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez, ambaye alivutiwa naye kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika wakati akiichezea Medeama dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, huku yeye akifunga bao pekee la timu yake lililowapa sare ya bao 1-1.
Mbali na kuichezea Medeama, Amoah pia yupo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20, ambacho kilitolewa na Senegal mwezi uliopita kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Zambia.
Mara baada ya kusaini mkataba huo, beki huyo kisiki anatarajia kuondoka nchini muda wowote kuanzia sasa kurejea Ghana kwa ajili ya kuichezea mchezo wake wa mwisho timu yake hiyo dhidi ya TP Mazembe, ukiwa ni wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika kesho Jumamosi, ambao una umuhimu mkubwa kwao kwani wapo kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kwa nusu fainali ya michuano hiyo.
Mara baada ya mchezo huo utakaofanyika Agosti 14 mwaka huu, beki huyo atarejea nchini kwa ajili ya kuanza kazi rasmi ndani ya uzi wa Azam FC, ambayo mwakani itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz, mara baada ya kusaini mkataba huo mbele ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, aliyekuwa sambamba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Medeama, Moses Armah na Mtendaji wa timu hiyo, James Essilifie, beki huyo alisema yupo tayari kwa changamoto zote za kuwania namba ndani ya kikosi hicho.
“Huu ni mkataba wangu wa kwanza kama mchezaji chipukizi nikijiunga na timu kubwa kama Azam FC, ninachohitaji mimi ni sapoti ya mashabiki na naomba waniombee, niko hapa kwa ajili ya kupigana na kufa kwa ajili ya klabu hii,” alisema Amoah.
Katika kipindi chote cha uchezaji msimu huu, Amoah amefanikiwa kufunga mabao matatu, mawili kwenye Ligi Kuu ya Ghana na moja akifunga katika Kombe la Shirikisho, aliloifunga dhidi ya Yanga.
Mghana huyo anaungana na staa mwingine aliyejiunga Azam FC akitokea Medeama, winga Enock Atta Agyei, ambaye ameshasaini mkataba wa miaka miwili tokea wiki iliyopita.
Usajili wa Kangwa
Staa mwingine wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, Bruce Kangwa, aliyefanya majaribio ya takribani wiki mbili, amelivutia benchi la ufundi la Azam FC na kupelekea kusaini mkataba rasmi baada ya viongozi kumalizana na mabosi wa Highlanders FC alilokuwa akiichezea timu hiyo.
“Ni jambo zuri kwangu kupata nafasi ya kucheza kwenye timu kubwa kama Azam FC, nashukuru sana kwa kunipa mkataba na jambo la kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani yeye ndio ameniwezesha kupata nafasi hii, haikuwa kazi rahisi unajua mtu unapotoka nje ya nchi kwenda kutafuta nafasi mahali inakuwa ni ngumu sana kushinda,” alisema Kangwa mara baada ya kusaini mkataba mbele ya Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Idd.
Beki huyo wa kushoto mwenye uwezo wa kucheza namba zote za upande wa kushoto ikiwemo pia nafasi ya mshambuliaji wa kati, alisema alipitia kipindi kigumu sana kwenye majaribio yake na kudai kuwa alifanya jitihada kubwa kadiri ya uwezo wake ili kupata nafasi hiyo.
“Hii haitaishia hapa kwangu, nitaendelea kufanya kazi kwa bidii na kuvuna kile klabu iliyopanga kupata kwa kufikia malengo, bado kuna mambo mazuri kutoka kwangu yanakuja cha msingi naomba mashabiki wa Azam FC waje kwa wingi na kutusapoti uwanjani,” alisema.
Kangwa hakuacha kuisifia Azam FC akisema kuwa: “Azam FC ni klabu profesheno zaidi, kila kitu kinapatikana ndani ya timu, unaweza kusema ni kama Manchester, Barcelona kutokana na namna inavyoendeshwa kwani kila kitu kipo na ni tofauti na klabu nyingine, hata kule Zimbabwe nilipotoka ni tofauti kabisa.”
Hadi anaondoka Highlanders, Kangwa ndiye aliyekuwa kinara wa ufungaji mabao kwenye Ligi Kuu ya Zimbabwe akiwa nayo saba hadi mzunguko wa kwanza wa ligi ukiwa umemalizika, ambapo alikuwa akichezeshwa kama mshambuliaji wa kati na mara nyingine kama winga winga wa kushoto.
Azam FC vs Ruvu
Wakati kesho Jumamosi saa 6.00 usiku ikiwa ni siku ya mwisho ya zoezi la usajili wa wachezaji, Azam FC itashuka tena dimbani kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, mkoani Pwani kujipima na wenyeji wao Ruvu Shooting.
Mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni, utatumiwa na Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben kama sehemu ya kukiangalia kikosi chake namna kitakavyokuwa kikitumia mbinu zake pale watakapokuwa wakicheza katika viwanja ambavyo havina ubora.
0 comments:
Post a Comment