Muda uliokuwa ukisubiri wa na watu wengi juu ya Zlatan sasa umewadia. Wiki nne zimeshapita tangu mchezaji huyo ambaye anaaminika kuwa na 'personality' kubwa kuthibitishwa kuwa mchezaji wa Manchester United. Jana ameonesha nini mshambuliaji anapaswa kufanya uwanjani baada ya kufunga goli lake la kwanza ndani ya nne ya mchezo katika mchezo wake kwanza dhidi ya Galatasaray akiwa kama mchezaji wa Man United.
Mchezo huo ulipigwa nchini kwao Sweden tena kwenye uwanja wa Gothenburg, hapana shaka kwamba mchezo huu ulikuwa unamhusu zaidi yeye.
Tayari ameshawaonjesha United ladha ya magoli ambayo amekuwa akifunga sehemu zote alizopita. Huyu ndiye Ibra Cadabra akiwa ndani ya jezi nyekundu ya Mashetani Wekundu.
Ibrahimovic kamwe hajawahi kusita kuuzungumzia uwezo wake uwanjani, sasa anaelekea kutimiza miaka 35 lakini ukimuangalia ndio kwanza anazidi kuwa kijana. Hatujui kama ligi ikianza itakuwaje, ni jambo la kujipa muda.
Ugumu wa ligi ya England unafahamika, mchezaji yeyote ambaye anataka kucheza ligi hii kwa mafanikio lazima awe na kasi, wepesi na hali ya upambanaji wakati wote. Hii inaleta utofauti na ligi nyingine nyingi za Ulaya. Ni kweli Zlatan ni mchezaji mwenye vitu vyote hivyo je, umri wake na ligi aliyotoka vinaweza kumpa mafanikio kwenye ligi ya England?
Jose Mourinho anaonekana kuwa na uwanja mpana wa kuchagua washambuliaji. Wakati wa Louis va Gaal alikuwa na ufinyu wa idadi ya washambuliaji lakini aliweza kuipeleka United Ligi ya Mabingwa, baadaye Europa na kuchukua Kombe la FA. Mourinho anaonekana kuwa makini zaidi na suala hili hasa kwa sasa anajua fika kwamba ligi ndiyo kipaumbele chake kikubwa.
Angewezaa kuwa na nafasi kubwa ya kuwatumia wachezaji kama Anthony Martial, Marcus Rashford na Wayne Rooney, kama namba tisa bila hata kuidhoofisha safu yake ya kiungo nyuma ya mshambuliaji wa mwisho. Lakini ujio wa Ibrahimovic na Henrikh Mkhitaryan umezidi kuleta utofauti mkubwa sana kwa United kutokana na kuongezeka kwa upana na thamani ya kikosi.
Ukubwa wa kikosi unazidi kumpa Mourinho nafasi kubwa ya kumtumia Zlatan kisawasawa kama mshambuliaji wa mwisho. Watu wengi wanataraji kuona kwamba timu inatengenezwa kupitia Zlatan kama mshambuliaji wa mwisho. Lakini swali linakuja je, ataweza kucheza kwa kiwango kile kile kama alichokuwa akikionesha muda wote kunako klabu ya Paris Saint-Germain au zaidi ya hapo?
Katika msimu wake wa mwisho kwenye klabu ya PSG, amefunga mabao 50 kwenye michezo 51, lakini ugumu na wingi wa mechi za England jumlisha na mapumziko finyu hakika vitampa wakati mgumu sana Msweden huyu. Inawezekana ndiyo maana Mourinho aliamua kumuongezea muda wa kupumzika kwa sasa ili isilete shida baadaye. Lakini ukweli ni kwamba Zlatan huyu si Zlatan yule wa miaka mitatu minne iliyopita kutokana na umri kuwa si rafiki kwake ukilinganisha na changamoto za EPL.
"Alikuwa bora sana kwenye Ligue 1 lakini sidhani kama anaweza kucheza michezo zaidi ya 30 msimu ujao hasa nchini England," alisema moja ya watu wa ndani wa PSG Loic Tanzi. "Mourinho atatakiwa amtunze vizuri lakini ugumu utakuja pale atakapokuwa akitaka kucheza kila mechi, hata michezo ile ya makombe ya ndani ya FA na Capital One,"
Zaidi ya majeraha yaliyomkumba msimu wa 2014-15, Ibrahimovic amecheza zaidi ya michezo 40 kwenye kila msimu tangu mwaka 2018. Hali hiyo inaweza kumpa kiburi Mourinho kuzidi kumchezesha kwa kadri anavyoweza, lakini kutokana na umri wake, hapo ndipo balaa linapoweza kutokea.
Mashabiki wengi wenye uchungu na Man United, wamekuwa wakihoji ujio wa Zlatan na maendeleo ya Rashford na mustakabali wa Martial. Lakini kiukweli hawatoathirika kwa kiasi kikubwa kwasababu kwa umri alionao Zlatan hataweza kucheza kila wiki kwa kiwango kile kile, hivyo makinda hao bado watakuwana nafasi kubwa ya kucheza.
Kwasababu ameletwa pale kwajaili ya kutoa mchango wa kuleta mataji klabuni hapo, basi itakuwa ni msaada mkubwa kwa Rashford, Martial na wengine kutokana na kujifunza mengi kutoka kwa legend huyo.
Jana amevaa jezi ya United kwa mara ya kwanza akiwa kama 'don' na kweli ameitendea haki jezi hiyo baada ya kufunga goli maridhawa na la ufunguzi katika mchezo huo.
Lakini yeyote anayetarajia Zlatan kucheza mechi 40 na zaidi kwa msimu na kufunga magoli mengi kama alivyofanya PSG, basi aangalie upya matumaini yake hayo. Ninachoamini kama atacheza mechi nyingi sana, basi ataishia kuwa na uchovu mwingi na kutofanya vizuri tena, lakini kama atafanyiwa 'rotation', basi makali yake bado yataendelea kuwatesa mabeki wa England.
Alipokuwa akiondoka PSG alisema: "Nilikuja kama mfalme na naondoka kama legend" na vile vile hivi karibuni alijibu madai ya Cantona ya suala la ufalme klabuni hapo kwa kwa kusema: "Siwezi kuwa mfalme wa Manchester United, nitakuwa Mungu wa Manchester."
Lakini bado halitakuwa suala la michezo mingi au magoli mengi ndio kumfanya Zlatan ama kuwa Mungu au sio pale atakapoondoka United. Isipokuwa uruthi na historia yake atakayoiacha ndiyo itakayomfanya achukuliwe kama anavyotaka ikiwa atafanya mambo yatakatowapendeza mashabiki wa klabu hiyo.
0 comments:
Post a Comment