Mshambulizi wa Italy ambaye ndani ya siku hizi mbili amejizolea umaarufu mkubwa Simone Zaza amesema kwamba penati aliyokosa kwenye mchezo wa robo fainali ya Euro dhidi ya Ujerumani itabaki kwenye akili yake katika maisha yake yote.
Akiwa ameingia katika dakika za mwisho za kipindi cha pili cha muda wa ziada kwa sababu maalum kwa ajili ya upigaji penati ambapo Ujerumani walishinda kwa penati 6-5 baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1, mshambulizi huyo wa Juventus alijikuta akipaisha penati yake juu baada ya kwenda kuipiga kwa madaha makubwa mithili ya mtu anayevizia kitu.
Zaza amesisitiza kwamba mara nyingi amekuwa akitumia staili ile na kuongeza kuwa, hata hivyo alimpoteza maboya kipa Manuel Neuer, lakini akikiri kwamba kamwe hatasahau penati ile katika maisha yake.
Akiongea na wanahabari wakati walipotua kwenye uwanja wa ndege wa Malpensa uliopo jijini Milan, Zaza alisema: "Nimekosa penati muhimu sana katika maisha yangu ya soka na itabaki kwenye kumbukumbu yangu kwenye maisha yangu yote hapa duniani. Naomba radhi sana kwa kuwaangusha Waitaliano.
"Mara nyingi nimekuwa nikipiga penati kwa mtindo ule na ndio maana nilishawishika kufanya vile kwa kuwa niliamini ningefunga. Nilimpelekea maboya Manuel Neuer, lakini kwa bahati mbaya mpira ulipaa.
"Itakuwa ni vigumu sana, lakini nitajitahidi kusahau . Ningependa Waitaliano wajue kwamba tulifanya kila jitihada ili kushinda.
"Naamini mashabiki wanatambua hilo kwamba tulifanya kila linalowezekana na nina furaha kwa mapokezi tuliyopata, nilijua wangeelewa hali halisi. Tumepata aibu isiyoelezeka kwani penati zile hakuna hata namna ya kuzizungumzia."
0 comments:
Post a Comment