NYOTA wa Kimataifa ya Zimbabwe, Bruce Kangwa, ametua nchini jana jioni tayari kabisa kufanya majaribio ya kujiunga na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC.
Kangwa anatokea kwa vinara wa Ligi Kuu nchini humo Highlanders FC na mpaka sasa ligi hiyo ikiwa mapumzikoni kufuatia kumaliza mzunguko wa kwanza, amefanikiwa kuwa kileleni kwa ufungaji bora akiwa na mabao saba.
Mzimbabwe huyo ameshachezea timu yake ya Taifa mechi 20 na mpaka sasa yupo kwenye kikosi hicho na anamudu kucheza nafasi tatu tofauti uwanjani, beki wa kushoto, winga wa kushoto na mshambuliaji.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya kuwasili nchini, Kangwa alisema kuwa amejipanga kufanya vizuri kwenye majaribio hayo.
“Ninajisikia vizuri sana nikiwa mchezaji wa kigeni kupata nafasi ya kujaribiwa na Azam FC, haya ni mafanikio makubwa sana, mchezaji wa Zimbabwe kuja hapa kwa majaribio ni mafanikio kwani kuna wachezaji wengi hata katika nchi nyingine, niko hapa kuonyesha uwezo wangu nina uhakika nitafanikiwa kusajiliwa,” alisema.
Kangwa, 27, anaungana na wachezaji waliokuwa kwenye majaribio, beki Mohamed Chicoto (Niger), washambuliaji Ibrahima Fofana (Ivory Coast), Fuadi Ndayisenga (Burundi) na Mossi Moussa Issa (Niger).
0 comments:
Post a Comment