Klabu ya Soka ya Ruvu Shooting imeamua kuachana na kocha wake mkuu Mkenya Tom Alex Timamu Olaba na badala yake kumtumia Seleman Mtungwe ambaye imemsomesha hadi Daraja B.
Olaba alijiunga na timu ya Ruvu Shooting msimu wa mwaka 2014 mzunguko wa pili baada ya aliyekuwa kocha mkuu Boniphace Mkwasa kuvunja mkataba na kuamua kwenda kuifundisha timu ya Yanga SC.
Wakati Olaba anaanza kuifundisha Ruvu Shooting aliikuta ikiwa na point 17, mpaka mwisho wa ligi Ruvu Shooting chini ya Olaba ilimaliza ikiwa nafasi ya 5, point 35.
Msimu wa 2015/16 Ruvu Shooting chini ya mwalimu Olaba haikufanya vizuri kwani ilishuka Daraja ikiwa na jumla ya pointi 29 japo kushuka kwake tunaweza kusema kulitokana na hujuma nyingi hasa katika mchezo wa mwisho wa msimu huo wa ligi ikicheza ugenini na mwenyeji Stand united kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga!
Olaba pamoja na kushuka kwa Ruvu Shooting, alikubali kushuka nayo hadi ligi Daraja la Kwanza akiahidi kuipandisha ahadi ambayo aliitekeleza.
Katika ligi hiyo ya FDL tulicheza kwa mafanikio makubwa tukiwa kundi B lenye timu nyingine saba ambazo ni Polisi Morogoro, Lipuli (Iringa), Kurugenzi (Iringa), Mji Njombe (Njombe), Mlale JKT (Songea), Kimondo (Mbeya) na Burkinafaso (Morogoro).
Tulimaliza ligi hiyo tukiwa na jumla ya pointi 33 tukiwa tumeshinda michezo 10 kati ya 14, tukipoteza mmoja dhidi ya Mlale JKT (1-0) na sare tatu, dhidi ya Njombe Mji (2-2), Kimondo (1-1) na Polisi Morogoro (0-0). Hayo yalikuwa mafanikio makubwa sana kwa timu ya Ruvu Shooting na Mwalimu Olaba.
Ruvu Shooting tunaheshimu sana mchango wa Olaba katika timu yetu na tunamheshimu sana Olaba, tutaendelea kumheshimu na kuamini kuwa ni miongoni mwa makocha bora katika ukanda huu wa nchi za maziwa makuu na Afrika!
Kila la Kheri Tom Alex Timamu Olaba, kocha makini, Mahili, mcheshi, mwenye weledi na akili nyingi katika kufundisha mpira.
Ruvu Shooting tunakukumbuka, tutaendelea kukumbuka kwa mema na mafanikio makubwa ndani ya timu yetu chini ya uongozi wako!
Mungu azidi kukubariki, kukupa afya, maisha marefu na mafanikio makubwa katika kazi yako ya kufundisha soka!
0 comments:
Post a Comment