YANGA imefanikiwa kumaliza utata wa kuendelea na kocha wao mkuu Hans Pluijm baada ya kumuongezea mkataba wa miaka miwili.
Mkataba wa Pluijm na Yanga ulifikia tamati mwezi mmoja uliopita ambao ndiyo umeipa klabu hiyo mafanikio ya kutwaa taji la ubingwa wa VPL mara mbili, Kombe la FA pamoja na kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.
Akizungumza na shaffihdauda.co.tz Pluijm amesema anafuraha ya kuendelea kuifundisha Yanga ambapo sasa anataka kuhakikisha anaendeleza kazi na mafanikio zaidi kwa Yanga kuweza kufika mbali katika mashindano ya CAF mwakani.
“Naipenda hii klabu sikuzote nimekuwa nikifanya kazi kwa kutanguliza heshima na mapenzi ambayo watu wa Yanga wamekuwa wakinionyesha, sasa nimeongeza mkataba ambao hata familia yangu ina furaha na hilo,” amesema Pluijm.
“Changamoto yangu kubwa sasa ni kuhakikisha Yanga inafanya mazuri zaidi kuzidi ya haya tuliyoyapata msimu huu naju haitakuwa kazi rahisi lakini hakuna namna lazima tupambane kila mmoja na nafasi yake kuweza kufikia malengo.”
Mkataba huo wa Pluijm ambaye wikiendi iliyopita aliibuka kuwa kocha bora wa msimu uliopita ameusaini mbele ya katibu mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit.
0 comments:
Post a Comment