Mpaka kufikia msimu wa nne wa ligi ya taifa, 1968, timu kali zilikuwa Yanga, Sunderland, Africans Sports na Cosmopolitan.
Mwaka huu, FAT iliamua kuachana na wazo la ligi ya kanda na badala yake ikafanyika ligi ya kawaida kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Baada ya kususa miaka yote mitatu ya kwanza, msimu huu Yanga ilipania kuchukua ubingwa na haikutaka utani hata kidogo. Ilishinda michezo yake yote ya mzunguko wa kwanza ukiwemo dhidi ya watani wao wa jadi, Sunderland Januari 13, 1968 kwa mabao 3-1.
Mzunguko wa pili haukuwa rahisi kwa Yanga kama ule wa kwanza kwani ilikutana na vichapo viwili vya vya kushtukiza kutoka kwa Africans Sports na Cosmopolitan.
Hata hivyo, mpaka hapo Yanga walikuwa juu kwenye msimamo wa ligi na tarehe 30/3/1968 walikutana na Sunderland, watani wao wa jadi.
Katika mchezo huo, mapema tu dakika ya 28, Kitwana Manara akaifungia Yanga bao la kuongoza.
Simba walipambana kugomboa bao hilo lakini hawakufanikiwa na baadaye, mmoja wa wachezaji wake, Emmanuel, akamshambulia mwamuzi, Jumanne Salum na mchezo ukavunjikia hapo.
FAT ikaamua mchezo urudiwe Juni Mosi, 1968...hii ilikuwa siku muhimu sana kwa Yanga kwani ndiyo siku ambayo walihamia kwenye jengo lao jipya la mtaa wa Mafia, lililojengwa kwa michango ya wanachama na mkopo wa benki ya nyumba.
Yanga waliitumia siku hii kuweka historia mbili; 1. Kuhamia jengo lao jioya na 2. Kumuadhibu mpinzani wao.
Katika mchezo huo, Yanga waliwanyanyasa Sunderland kama walivyotaka. Mapema kipindi cha kwanza, Maulid Dilunga aliifungia Yanga mabao mawili ya mikwaju ya adhabu ndogo.
Salehe Zimbwe aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awadh Gessani, aliiandikia Yanga bao la tatu kwa staili ya kukera na kuudhi kwani aliwapiga chenga walinzi wawili wa Sunderland na kumvisha kanzu golikipa, Mbaraka, kabla ya kufunga kwa kichwa.
Maulid Dilunga, mfungaji wa mabao mawili ya kwanza, alimtengenezea bao Kitwana Ramadhan Manara na kuiandikia Yanga bao la nne. Mpaka hapo, Sunderland wakakata tamaa.
Kuona hivyo, Yanga wakaanza mchezo wa mizaha na masihara na kuzidi kuwaudhi wachezaji wa Sunderland. Yanga wakawa wanakokota mpira kutoka golini kwao mpaka kwa Sunderland halafu wanarudi nao mpaka kwao na kumpasia kipa wao Elias Michael ambaye aliudaka na kuurusha kwa ndugu zake huku wakifanya dhihaka kwa wachezaji wa Sunderland kwa kuwacheka na kujifanya kama wanapandisha soksi au kuvua jezi au bukta.
Dakika za mwisho kabisa, Saleh Zimbwe tena akarudi nyavuni kwa Sunderland na kuhitimisha ushindi wa Yanga wa mabao 5-0.
Ushindi huu uliihakikishia Yanga ubingwa wao wa kwanza wa taifa.
Zaka Zakazi
0718171079
0 comments:
Post a Comment