Tuesday, July 19, 2016

Mwaka 1967 ulikuwa msimu wa tatu wa ligi ya taifa yaani mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya taifa.

Msimu huu ulishuhudia mabadiliko makubwa. Kwa mara ya kwanza, timu ziliingia kwenye ligi kwa kupanda daraja na zile zilizomaliza nafasi tatu za chini msimu uliopita, zilishuka daraja. Timu zilizoshuka daraja ni:

1. Tobacco (Sigara) iliyomaliza katika nafasi ya nane
2. Manchester United ya Tanga iliyomaliza katika nafasi ya tisa
3. Sunderland ya Tanga iliyomaliza katika nafasi ya mwisho.

FAT iliamua kwamba mwaka huu ligi ichezwe kwa  mfumo wa vituo vitakavyogawanywa kikanda, kanda sita ziligawanywa;

Kanda A- Tabora, Kigoma na Shinyanga.

Kanda B - Kilimanjaro, Singida na Arusha

Kanda C - Dodoma, Iringa na Mbeya

Kanda D - Mwanza, Mara na Bukoba

Kanda - E - Mtwara na Ruvuma

Kanda - F - Morogoro, Tanga na Pwani

Nia ilikuwa mabingwa wa kila kanda waje Dar Es Salaam kwa fainali.

Lakini kiuhalisia, mfumo huu ulikuwa mgumu kutekelezeka kutokana na uduni wa viwanja vya mikoani na matayarisho hafifu. Mpaka mwaka unakaribia kumalizika, hakuna hata kanda moja iliyomaliza mashindano yake. 

Mwaka huo ndiyo kwa mara ya Tanzania ilitakiwa kupeleka jina la bingwa wake makao makuu ya CAF Cairo Misri ili aingizwe kwenye ratiba ya klabu bingwa Afrika kwa mwaka 1968.

Kwa kuwa bingwa wa Tanzania alikuwa hajapatikana na ikaonekana vigumu kupatikana kwa mfumo wa kanda, FAT ikaandaa mashindano mengine ya haraka haraka 'ligi ndogo ya mtoano' ili kuharakisha kupatikana kwa bingwa. Hii ilikuwa tayari mwezi Novemba.

Timu zilizotakiwa kushiriki zilikuwa;

1. Coastal Union ya Tanga
2. TPC ya Moshi Kilimanjaro
3. Cooperative United ya Mwanza
4. Mwadui FC ya Shinyanga
5. Yanga ya Pwani
6. Sunderland ya Pwani
7. Cosmopolitan ya Pwani
8. African Sports ya Tanga

Ligi hii ndogo ilizua malumbano kutoka kwa 'wakubwa wawili', Sunderland na Yanga. Sunderland walikataa kushiriki wakisema hakuna haja ya mashindano hayo na badala yake FAT ipeleke CAF jina lao kwa sababu wao ndiyo mabingwa wa msimu uliopita. FAT ikatupilia mbali madai ya Sunderland ikisema sheria inataka bingwa apatikane kila mwaka.

Yanga nao waligoma kushiriki 'ligi ndogo' wakisema hawana wachezaji kwani wachezaji wao wengi walisafiri na timu ya taifa iliyoenda Kinshasa 'Zaire' kwa Kombe la mataifa ya Afrika na wakitoka huko waunge moja kwa moja Nairobi Kenya kwa Kombe la Gossage (siku hizi Kombe la CECAFA).

FAT ikaachana na 'vidume hao' na kuchukua timu nyingine badala yake. Timu hizo zilikuwa Tambaza ya Pwani na Police ya Pwani pia. Timu zilizoshiriki 'ligi ndogo' zilikuwa kama ifuatavyo:

1. Cosmopolitan  ya Pwani
2. Mwadui FC ya Shinyanga
3. Coastal Union ya Tanga
4. TPC ya Moshi
5. Cooperative United ya Mwanza
6. African Sports ya Tanga
7. Tambaza ya Pwani
8. Police ya Pwani

Baada ya mtoano, timu mbili za Cosmopolitan na Coop. United ziliingia fainali iliyopangwa kufanyika Disemba 2, 1967 kwenye uwanja wa Ilala ( siku hizi Karume)

Siku ya fainali, saa chache kabla ya mchezo, Coop. United wakatuma taarifa kwa FAT kwamba hawatacheza siku hiyo kwa sababu wachezaji wao wengi waliumia kwenye nusu fainali dhidi ya African Sports.

FAT wakasisitiza kwamba lazima fainali ifanyike siku hiyo kwani kesho yake mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ulikuwa ukitarajiwa kuanza na watu wengi wa dini ya Kiislamu wakiwemo wachezaji wangefunga.

Muda wa mchezo, Cosmo wakaingia uwanjani lakini Coop. United hawakutokea. Mwamuzi akamaliza mchezo na Cosmo wakatawazwa mabingwa wa Tanzania.

Jina la bingwa mpya, Cosmopolitan, likatumwa Cairo na timu hiyo ikawa mwakilishi wa kwanza wa Tanzania kwenye mashindano ya Afrika.

Mchezo wao wa kwanza ulikuwa dhidi ya timu kutoka Somalia na kupata sare ya 0-0 nyumbani lakini ikashindwa kwenda kwenye mchezo wa marudiano kutokana na ukata.

Zaka Zakazi
0718171078

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video