Unaikumbuka hii ya ukurasa wa mbele wa gazeti la Corriere dello Sport ukiwa umepambwa na bendera yenye picha ya Balotelli?
Na hii ya dereva aliyekuwa akiishi karibu na Piazza del Popolo huko jijini Rome aliyekuwa ameandika kwenye basi lake Super Mario.”? Huyu ndiye Mario Balotelli aliyekuwa anafahamika na sio huyu wa sasa ambaye pengine amekuwa kama 'mbwa koko'. Mbwa asiye na makali hata pindi amwonapo adui.
Miaka minne iliyopita, mshambuliaji huyu mtukutu mwenye asili ya Kiafrika alikuwa ndio mwiba mchungu kwa Wajerumani. Kwanini mwiba mchungu?Unayakumbuka magoli mawili waliyofungwa Ujerumani dhidi ya Italy kwenye nusu fainali ya Euro mwaka 2012? Sasa yule ndiye alikuwa Balotelli halisi.
Goli la pili alifunga kwa shuti kali na kuvua shati huku akitunisha misuli yake na miguu kuitanua akiwa na uso wa mbuzi hacheki na mtu. Kuanzia usiku huo mpaka kesho yake picha zake zilisambaa ulimwengu mzima huku akipewa sifa kedekede. Huyu ndiyo Super Mario Barwuah Balotelli
Sasa ni miaka minne imepita, Balotelli amekuwa si yule tena. Amebaki jina tu, hana nafasi kila sehemu aendayo.
Kutokuwa kuwa mshambuliaji tegemezi kwa taifa lake kwenye Michuano ya Ulaya, mpaka kuwa mshambuliaji asiyefikiriwa Liverpool. Hivi karibuni Liverpool walikuwa na michezo ya kirafiki dhidi ya Fleetwood na Wigan, lakini hata kwenye michezo hiyo Klopp Balotelli hakupewa fursa wala hata ya kucheza kwa dakika tano tu.
Akiwa na umri wa miaka 25 kwa sasa. Ana taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ameshinda Serie A mara 3, Ameshinda taji la EPL mara moja. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa mchezaji mwenye umri mdogo kabisa kama wake.
Bado anaweza kuwa mchezaji muhimu Liverpool, anaweza kuwa mchezaji mwenye madhara makubwa, vile vile mchezaji mwenye maamuzi kwenye timu.
Lakini si hivyo kwa Balotelli, kwa sasa amekuwa mchezaji asiye na malengo na wala asiye na mwamko tena kama mchezaji ambaye umri wake umekwenda.
Mustakabli wake kunako klabu ya Liverpool haujulikani huku mpaka sasa kukiwa hakuna vilabu vyovyote vikubwa ambavyo vimeonesha kumhitaji.
Ni Sampdoria na Crotone tu kutoka Serie A ndio wameonesha nia ya kuhitaji huduma yake lakini hata hivyo hawajatuma ofa rasmi. Sasa unaweza kushangaa kwamba mchezaji wa hadhi ya Balotelli na umri wake wa miaka 25 akacheze Sampdoria, klabu ambayo inapigana kutoshuka daraja, klabu isyojua hata ladha ya Uefa Europa!!.
Amerudi Liverpool baada ya msimu uliopita kuutumia kwa mkopo akiwa na AC Milan. Alihitaji kuendelea kubaki Milan lakini nao wameoneshwa kutokuwa na uhitaji naye. Huyu si Balotelli ninayemfahamu mimi wa kukataliwa hata na AC Milan ambao kwa sasa wako 'dhofu lhali'.
Yale maandishi yake ya ‘Why Always Me?’yamegeuka kuwa ‘Why always Not Me?’
Kuna wakati kiungo maestro wa Italy Andrea Pirlo alisema ameshawahi kucheza na washambulizi bora duniani na Balotelli kwa namna anavyocheza ana kila sifa ya kuwa mshambuliaji bora duniani.
"Lakini kwa sasa nadhani ni mahali ambapo anapaswa kuwa kutokana na yake aliyoendekeza kuyafanya," Pirlo anasema.
Kuna wakati fulani aliyekuwa nahodha wa Liverpool Steven Gerrard amewahi kusema: "Balotelli ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa mno na mwenye sifa ya kuwa mshambuliaji bora duniani, lakini kamwe hawezi kufika huko kutokana na mwenendo wa tabia zake na watu wanaomzunguka.
“Mara nyingi Balotelli anataka kuwa midomoni mwa watu, azungumzwe kila mara…
“Hajitumi kwa bidii kwenye maisha yake ya kila siku. Ukipambana na Balotelli basi we kubali kushindwa. Anafanya mambo mengi sana ya ajabu."
Kuna wakati aliyewahi kuwa kocha wa Manchester City Roberto Mancini ambaye alimfanya Balotelli kama mwanaye alinukuliwa akisema: "Nadhani ni muhimu kuanza kuona kwamba Balotelli anaanza kufikiaria juu ya soka na sio mambo mengine yanayomzunguka.
Si kana kwamba ni watu wachache tu wanaopenda mafanikio ya Balotelli. La hasha, bali wengi wao wanaogopa kufanya naye kazi kutokana na mwenendo wa matendo yake.
Kama unakumbuka vizuri, aliposajiliwa na Liverpool misimu miwili iliyopita, alikiri kwamba angekuwa mtuliwa na kuachana na mambo yote na kuzingatia kilichmleta klabuni hapo.
Haikuchukua muda muda baada ya kauli yake hiyo akaanza mikasa yake baada ya kukorofishana na aliyekuwa nahidha wa timu hiyo Steven Gerrard, kuna wakati alisahau kama kuna ratiba ya timu yake kucheza na kujiwekea ratiba zake zingine. Haya ni miongoni mwa mambo machache tu ambayo yamemfanya Balotelli kufika hapa alipo kwa sasa.
Alikuwa akiendekeza mambo binafasi ambayo yalikuwa yanaleta ukakasi kwa kwenye kikosi cha wekundu hao wa Anfield.
Balotelli amerudi tena kwenye kikosi cha Lverpool msimu huu, tayari kocha wa Liverpool Jurgen Klopp ameshatanabaisha kwamba, mchezaji huyo atafute tu timu nyingine maana hayupo kwenye mipango yake licha ya kusema maneno mazuri kwake.
Klopp alinukuliwa akisema. “Nimesikia mengi sana juu yake tangu nilipowasili hapa,"
“Tangu amerudi hapa, amekuwa ni kijana mzuri na siwezi kusema tofauti kuhusu yeye.
Kauli hii ya Klopp ina ina maana kubwa sana kwa Balotelli, pengine akionesha juhudi zaidi anaweza kubaki hapo na kuwa Balotlli yule wa Man City na Inter Milan enzi za Mourinho.
Mario Baloteli anatoa fundisho kubwa sana juu ya suala la kuzingatia nidhamu katika shughuli yoyote ile. Bila nidhamu hata kama una kipaji au akili nyingi kiasi gani basi unaweza usifanikiwe kwa kiasi ambacho wengi walitarajia.
0 comments:
Post a Comment