Baada ya mbilinge-mbilinge za Michuano ya Euro kumalizika sasa tunashuhudia mameneja mbalimbali wapya na wale wa zamani wakianza kuvinoa vikosi vyao kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi tofauti-tofauti.
Ligi ambayo watu wengi wanashauku na kuona ikianza ni ligi ya England, sababu ziko wazi tu, kwanza msisimko wake na kubwa zaidi msimu huu kusheheni mameneja wenye profile (hadhi) kubwa na hivyo kuwapa watu shauku ya kuona kitakachojiri.
Maswali bado ni mengi je, Arsenal Wenger ataingia sokoni kupambana kwa ajili ya kupata straika wa kumpatia ubingwa alioukosa kwa muda mrefu au kuendelea kuwategemea Giroud, Sanogo na Mjapan Asano Takuma ambao kimsingi sidhani kama wataiweza shughuli ya EPL.
Vita vya timu kutokana na uhasimu wa makocha utakuwa ni chachu kubwa ya utamu wa ligi. Pep Guardiola, Jurgen Klopp, Wenger na Mauricio Pochettino watakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kuepuka vipigo hasa kutoka kwa timu ndogo-ndogo. Unajua kwanini nimewataja makocha hawa....sababu kubwa ni kwamba hawa ni makocha ambao wanaamini sana kwenye falsafa zao bila ya kujali mchezo unaendaje licha ya kwamba kwa upande wa Wenger hii ni kesi nyingine kutokana na kuamini kutobadilika pale anapoamua kusimamia anachokiamini.
Kwa upande wa Jose Mourinho na Antonio Conte, hawa ni makocha ambao wengi wetu tunafaamu aina yao ya soka. Wanaamini zaidi katika kuzuia kuliko kushambulia hasa wanapokutana na timu kubwa na zenye kushambulia kwa kasi. Lakini nao pia wamejinasibu msimu huu kucheza soka la kushambulia kwa kasi ya hali ya juu kwa ajili ya kupata matokeo.
Leicester City walionekana kuwa na hatari kubwa msimu uliopita hasa kutokana na muunganiko mzuri wa wachezaji kama N'Golo Kante, Riyad Mahrez, Drink Water pamoja na Jamie Vardy. Lakini sasa kuondoka kwa Kante kwenda Chelsea huku Mahrez akihusishwa kuondoka pia na kuhamia moja ya vilabu vikubwa inaonekana kuwa janga sasa kwa Leicester. Hili ni janga ambalo linaweza kuwapa wakati mgumu sana Leicester vinginevyo kuwe na juhudi za makusudi kutoka kwa kocha mkongwe na mzoefu wa ligi mbalimbali Muitaliano Claudio Rannieri.
Vipi kuhusu vita ya moja ya mahasimu mahasimu wakubwa kuwahi kutokea katika ulimwengu wa soka? Hawa si wengine bali ni Guardiola na Mourinho.
Ni kweli Mourinho na Guardiola walikuwa na uhasimu mkubwa wakati wakiwa La Liga wakati huo Mourinho akiwa na Madrid huku Guardiola akiwa na Barcelona. Lakini hiyo ilikuwa wakati huo, vipi kuhusu sasa? Tangu wawili hao wapewe majukumu ya kuvinoa vilabu vya jiji la Manchester, wamekuwa kimya kila mmoja akiogopa kurusha kombora kwa mwingine pengine mpaka pale ligi itakapoanza rasmi na kuona mwenendo utakavyokuwa.
Manchester United chini ya Louis Van Gaal ilionekana kuwa klabu iliyokosa ari, wakicheza soka la kushambulia lakini lisio na madhara kwa wapinzani wao. Mafanaikio yake makubwa klabuni hapo ni ubingwa wa FA aliowapa msimu uliopita. Ikumbukwe alirithi mikoba ya David Moyes ambaye pia alitimuliwa baada ya kutoipa timu hiyo mafanikio. Amekuja Mourinho sasa, mtu ambaye anasifika kwa kutaka mafanikio kwa mbinu yoyote ile kwenye kila klabu aliyopita, licha kwamba kwa sasa anakutana na presha kubwa mno ambayo pengine hajawahi kuipata.
Mourinho ana kazi kubwa ya kufanya, ikumbukwe kuwa mwishoni mwa msimu uliopita wa ligi mashabiki wa United walifikia hatua ya kumkejeli Van Gaal kwa kumuimbia "Sisi ni Man United na tunataka kushambulia." Sasa hii ni kusema kwamba Mourinho ana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba United wanarejea katika kucheza soka lao la kushambulia na kujijengea heshima kubwa kama ilivyo kwa kocha wa zamani wa klabu hiyo Sir Alex Ferguson.
Juhudi zake za kutaka kufanikisha hayo zimeanza kuonekana baada ya kuleta wakali wawili kwenye safu yake ya ushambuliji....si wengine bali ni straika mwenye kiburi na uwezo mkubwa uwanjani Zlatan Ibrahimovic ambaye alimaliza mkataba kunako klabu ya PSG pamoja na kiungo mshambuliaji kutoka Borussia Dortmund Henrikh Mkhitaryan. Na kama atafanikiwa kumleta Paul Pogba ambaye ada yake itakuwa imevunja rekodi ya usajili wa pesa nyingi duniani, basi atakuwa amejitengenezea mazira mazuri ya kumkata maini hasimu wake Pep Guardiola.
Kwa upande wa Guardiola anaonekana kutokuwa bize sana kwenye usajili licha ya kumnasa Ikay Gundogan, amekuwa bize sana kuhakikisha anaingiza falsafa yake kwenye timu hiyo ambayo haikufanya vizuri kwenye ligi ya msimu uliopita licha ya kufika nusu fainali ya Klabu Bingwa. Kikubwa ambacho Pep anapaswa ili kuwafurahisha mabosi wake waarabu wa Abu Dhabi ni kuhakikisha anashinda taji la Champions League, kitu ambacho ameshindwa kufanikiwa kwenye klabu ya Bayern Munich pamoja na kuwa na kikosi bora kabisa.
Hata hivyo chagizo la utamu wa uhasimu kati ya Guardiola na Mourinho umeongezwa na uwezo aliounesha Conte kwenye Michuano ya Euro wakati akiwa na timu yake ya Italy. Muitaliano huyo ambaye alionekana kuwa na ghadhabu pale maelelezo yake yasipofuatwa ipasavyo, aliiongoza Italy kufika mpaka nusu fainali licha ya kutocheza soka lenye kuwatuvia wengi bali soka la matokeo. Conte naye kaanza kazi yake, amefanikiwa kuinasa saini ya Kante kuimarisha safu yake ya kiungo na vile vile mshambuliaji kinda rais wa Ubelgiji Michy Batshuayi.
Akili kubwa aliyotumia Conte ni kumbakisha beki mkongwe wa klabu hiyo John Terry ambaye allikuwa aondoke baada ya msimu uliopita. Dhumuni la kufanya hivyo ni kupata wasaa wa kujua mabo mengi kutokana na uzoefu wa beki huyo kunako klabu hiyo na Ligi ya England kwa ujumla.
Vilabu vingine kama Arsenal, Spurs and Liverpool wanaonekana wanautaka ubingwa wa EPL lakini wanaonekana kutokuwa na hamasa ya kuchukua wachezaji wa kaliba ya ubingwa.
Arsenal wamekuwa vinara wa kuhusishwa na uhamisho wa wachezaji bora kila msimu. Usajili wao mkubwa ni kumleta Mswisi Granit Xhaka. Ikumbukwe kuwa Arsene Wenger mwishoni mwa msimu uliopita alizomewa na mashabiki wa timu hiyo, lakini anaonekana kuwa mkaidi na kuleta watu wa kuleta matokeo chanya hasa safu yake ya ushambuliaji.
Liverpool kwa upande wao chini ya Klopp, wameshafanya usajili wa maana mmoja tu baada ya kumleta Msenegali aliyekuwa akikipiga Southampton Sadio Mane kwa ada ya dola milioni 50 huku akibaki kimya kwenye safu yake ya ushambuliaji kwa kuwategemea Christian Benteke Mario Balotelli ambaye amesema hana mpango naye bila kusahau Mbelgiji Divock Origi.
0 comments:
Post a Comment