Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta akijaribu kumtoka mchezaji wa Misri Abood Abdulrahman Amed wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2017
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshindwa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika maarufa kama AFCON baada ya kukubali kufungwa bao 2-0 kwenye uwanja wa taifa matokeo ambayo yamezima kabisa ndoto za watanzania kuiona timu yao kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya mataifa.
Awali Stars ilikuwa inahitaji ushindi angalau wa magoli 3-0 ili kuweka hai mipango ya kwenda Gabon kabla ya kukutana na Nigeria September mwaka huu mchezo ambao Stars ilitakiwa kushinda pia kwa idadi nzuri ya magoli ili kufanikiwa kufuzu.
Mohamed Salah anayekipiga Sirie A kwenye klabu ya AS Roma, aliifungia Misri bao la kuongoza dakika mbili kabla ya half-time kwa kuunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa nje kidogo ya eneo la penati.
Kipindi cha pili Stars ilirudi kwa nguvu kwa kutaka kusawazisha bao hilo lakini mambo yalikuwa magumu kutokana na kushindwa kuzitumia nafasi muhimu zilizopatikana.
Mbwana Samata alikosa mkwaju wa penati ambao kama angepata ungeirejesha Taifa Stars mchezoni kwa matokeo ya goli 1-1, dakika chache baadaye Misri waliongeza goli la pili kupitia kwa Salah aliyetumia makosa ya safu ya ulinzi ya Stars, goli ambalo liliikata maini Stars kwa kuiongezea mlima mkubwa iliotakiwa kuupanda.
Matokeo hayo yanaifanya Misri kuongoza Kundi G kwa kufikisha pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote kwenye kundi hilo.
Nigeria ipo nafasi ya pili kwenye kundi hilo ikiwa na pointi 2 wakati Stars ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi yake moja. Misri imeshamaliza mechi zake nne kwenye Kundi G ikiziacha Tanzania na Nigeria zikiwa na mchezo mmoja utakaozikutanisha zenyewe kwa zenyewe mchezo ambao utakuwa ni wa kukamilisha ratiba.
Fahamu dondoo muhimu
- Misri inafuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon mwaka 2017 baada ya kushindwa kufanya hivyo katika michuano mitatu iliyopita. Mara ya mwisho kushiriki michuano hiyo ilikuwa mwaka 2010 ilipoibuka bingwa wa mashindano hayo.
- Michezo mitatu iliyopita (kabla ya leo) ambayo imezikutanisha Tanzania na Misri, Stars imefungwa katika michezo yote. November 4, 2009 Misri iliifunga Stars bao 5-1, kisha ikaifunga tena bao 5-1 kwenye mchezo uliochezwa January 5, 2011 na mchezo wa mwisho Stars ikakubali tena kipigo cha magoli 3-0 (Mechi zote Stars ilicheza ikiwa ugenini. Leo tena June 4, 2016 Stars ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani imefungwa na Misri kwa magoli 2-0.
- Licha ya kuwa mabingwa watetezi wa kombe la mataifa ya Afrika, mwaka 2012 Misri ilishindwa kufuzu kwenye fainali za mataifa ya Afrika zilizofanyika Gabon na Equatorial Guinea. Wakashindwa tena kufuzu kwa fainali zilizofanyika mwaka 2013.
- Kwa mara ya tatu mfululizo, Misri ilishindwa kukata tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika Equatorial Guinea mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment