Mlinzi wa kulia wa Tanzania Prisons 'Wajelajela', Salum Mashaka Kimenya amesema yuko tayari kujiunga na klabu ya Simba SC endapo itaweka mezani dau la kuridhisha.
Akizungumza na MPENJA SPORTS jioni hii, Kimenya ameeleza kwamba Simba imeonesha nia ya kumsajili na tayari maafisa wake wamekuwa wakiwasiliana naye mara kwa Mara, lakini kitita wanachoweka mezani hakimshawishi kukubaliana nao.
"Nimekuwa nikizungumza nao sana (Simba), sina tatizo lolote kusaini kwao, ila nataka watoe fedha ya kuridhisha". Alifafanua Kimenya.
Pia nyota huyo mwenye uwezo wa kupanda na kupiga krosi alibainisha kuwa soka ni Kazi yake kwahiyo haoni shida kuihama Prisons kama timu nyingine inaweka vizuri maslahi yake.
"Mimi najiona nina thamani Kubwa na ndio maana Simba wanataka nikafanye Kazi. Kiukweli bila milioni 50 sidhani kama naweza kusaini timu yoyote". Alisisitiza Kimenya.
Taarifa kutoka vyanzo vya ndani zinaeleza kuwa Simba SC wameweka mezani milioni 30 wakiitaka saini ya Kimenya ambaye ni askari Magereza.
Wekundu hao wa Msimbazi wanahaha kutafuta beki wa kulia baada ya kuachana na Hassan Kessy aliyetimkia Yanga sc baada ya kumaliza mkataba wake, huku mlinzi mwingine Emery Nimuboma akiwa hatarini kuachwa majira haya ya kiangazi ya Usajili.
Hata hivyo, kamati ya Usajili ya Simba chini ya mwenyekiti wake, Zakaria Hanspope imesema Msimu huu usajili wao ni wa kimya kimya tofauti na mahasimu wao Yanga sc ambao wanaweka mambo yao hadharani.
0 comments:
Post a Comment