Na Yahaya Mohamedy
Baada ya mwenyekiti wa Yanga na mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji kuwasimamisha uanachama baadhi ya wanachama aliodai kumuhujumu pamoja na wale waliochukua fomu TFF kugombea nafasi mbalimbali.
Mmoja wa waliohusishwa na kusimamishwa uanachama ni Aron Nyanda ambaye alichukua fomu katika ofisi za TFF kwa ajili ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Akizungumza na mtandao huu Nyanda amesema hajapata taarifa rasmi juu ya kufutwa kwake uanachama: “Unajua timu yetu inaendeshwa kwa kufuata utaratibu na hizi taarifa unazoniambia hapa nimezisikia tu kwenye vyombo vya habari lakini sijapewa taarifa rasmi”, alisema.
Nyanda ameongeza kwamba kwa mafanikio iliyoyapata Yanga msimu huu ni kutokana na ushirikiano wa viongozi, mashabiki na wanachama hivyo kitendo cha watu kujitokeza kuchukua fomu ni katika hali ya kuijenga zaidi klabu.
“Unajua sote tuna lengo moja la kuijenga timu yetu na unakumbuka mimi nilichukua fomu siku ya Jumanne siku ambayo ilikua ya mwisho kuchukua fomu kwa mujibu wa tangazo la TFF kwa maagizo ya BMT na hakuna tamko lolote lililokua limetolewa na Yanga”, amesema Nyanda.
Kutokana na mkanganyiko huo wa TFF na klabu ya Yanga juu ya uchaguzi huo, Nyanda amesema bado hajajua kama atachukua fomu klabuni kwani anachokiona hivi sasa ni pande zote tatu kukutana na kumaliza tofauti zilizopo.
“Siwezi kusema kwamba ntaenda kuchukua fomu klabuni maana kunaonekana kuwepo na mvutano, lakini ushauri wangu ni pande zote kwa maana ya BMT, TFF, na Yanga zikutane zimalize tofauti zinazoonekana kisha uchaguzi ufanyike kwa amani, na siyo lazima mimi nigombee anaweza kugombea mtu yoyote ili mradi Yanga yetu isonge mbele” aliongeza Nyanda.
Nyanda ni miongoni mwa wanachama 9 waliotangazwa kusimamishwa uanachama kutokana na kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika ofisi za TFF pamoja na mwanachana Msumi aliyedaiwa kupanga njama za kumuhujumu Manji.
Tangazo la kuwasimamisha uanachama lilitolewa Alhamisi na Yusuf Manji alipojitokeza kuchukua fomu ya kuomba nafasi ya uenyekiti makao makuu ya klabu ya Yanga sambamba na makamu wake Clement Sanga.
Credit:Shaffihdauda
0 comments:
Post a Comment