Baada ya suluhu ya mchezo wa kwanza wa kundi B, Brazil wametoa kipigo cha mbwa mwizi dhidi ya Haiti baada ya kuwanyuka magoli 7-1 katika muendelezo wa mashindano ya Copa America Centenario mchezo ulifanyika katika uwanja wa Orlando, Florida.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa ni Philippe Coutinho ambaye alipiga hat-trick.
Iliwachukua dakika 14 tu za Brazil kuandika bao la kwanza kupitia kwa Philippe Coutinho. Baadaye akafunga tena bao la pili dakika ya 29 baada ya kupata pasi murua kutoka kwa Jonas ambaye pia aliipata kutoka kwa Dani Alves.
Renato Augusto aliiandikia Brazil bao la tatu katika dakika ya 35 kwa kichwa kutokana na pasi nzuri ya Alves baada ya uzembe wa wazi wa kipa wa Haiti Johnny Placide.
Beki wa Arsenal Gabriel Paulista alizidi kushindilia msumari wa mto kwa Haiti baada ya kufunga goli la nne mnamo dakika ya 59
Lucas Lima akaifungia Brazil goli la tano dakika ya 67 baada ya pasi mahiri ya Dani Alves ambaye alikuwa ndiyo 'assists master ' kwenye mchezo huo.
Haiti walipata goli lao la kufuia machozi dakika ya 70 kupitia kwa James Marcelin ambaye alipiga mpira uliomgonga kipa wa Brazil Alisson Becker na kutinga wavuni.
Augusto alifunga goli lake la pili katika mchezo huo na sita kwa Brazil mnamo dakika ya 86. Coutinho alikamilisha hat-trck yake baada ya kufunga goli zuri kabisa katika dakika ya 90 na kufanya idadi ya magoli kuwa 7-1. Mchezo ujao Brazil wataivaa Peru wakati Haiti watakuwa na kibarua dhidi ya Ecuador. Matokeo mengine ya kundi hilo, Ecuador wametoshana nguvu na Peru baada ya kufungana mabao 2-2.
Dondoo muhimu
- Idadi ya magoli 7-1 dhidi ya Haiti ni ushindi ambao unafanana na kipigo cha mabao 7-1 kutoka kwa Ujerumani katika michuano ya kombe la dunia iliyofanyika mwaka 2014 nchini kwao.
- Hat-trick ya Coutinho kwenye Copa America ni ya kwanza tangu mwaka 2007 tangu Robinho alipofanya hivyo.
- Goli la nne la Coutinho katika michuano hiyo hiyo linaashiria kwamba magoli yote manne ya Barzil kati ya sita ya mwisho katika michuano hii yamefungwa ndani ya dakika 15 za kwanza (3 mwaka 2015).
0 comments:
Post a Comment