DONALD Ngoma straika wa Yanga ndiye aliyefunga bao moja la kichwa la kuisawazishia Yanga dhidi ya Al Ahly ya Misri, kwenye mchezo wa marudiano wa klabu Bingwa Afrika jijini Alexandria.
Bao hilo ambalo lilitokana na krosi safi ya beki, Juma Abdul, sasa ndiyo limewachengua miamba wa soka nchini Misri klabu pinzani za Al Ahly na Zamalek.
Klabu hizo kubwa na vigogo katika soka la Afrika zenye makao yake jijini Cairo, zinapigana vikumbo hivi sasa kila moja kuhitaji huduma ya Ngoma na kwamba zinakwenda resi kuzidiana kete.
Taarifa zinasema kwamba maofisa wa klabu hizo wameanza upekuzi wa kujua namna gani wanaweza kumuingia nyota huyo huku wengine wakitaka kujua katika klabu aliyotoka ya FC Platinum.
Taarifa hizo zinasema kwamba, Zamalek wameulizia kwa FC Platinum juu ya mkataba wa Ngoma na Yanga na kwamba wameanzia huko na kisha wakatua kwa Wanajangwani kwa mazungumzo rasmi.
Ngoma amezivutia klabu hizo baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu kwenye mchezo wa Klabu Bingwa Afrika uliokutanisha klabu yake ya Yanga na Al Ahly ambayo baadae Yanga waliondolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-2.
Akizungumza na BINGWA, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Jerry Muro alithibitisha Ngoma kutakiwa na klabu hizo na kusema kuwa kwa sasa wanasubiri ofa tu kutoka kwenye timu hizo.
“Ni kweli tulizungumza na wawakilishi wa timu hizo ambao walionekana kumuhitaji mshambuliaji wetu na wameahidi kuleta ofa ndani ya wiki moja, na sisi tunasubiri kuona timu gani itakuwa na ofa nzuri,” alisema Muro.
Ngoma aliyefunga mabao 17 msimu huu pia awali alitakiwa na timu kutoka Afrika Kusini na klabu mbili za Malaysia lakini Yanga walipotezea ofa za timu hizo.
Kwa sasa staa huyo yupo nchini Zimbambwe kwenye mapumziko kabda ya kurejea kwenye maandalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo Yanga wameingia kwenye hatua ya makundi.
0 comments:
Post a Comment