KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imepongezwa kwa kuandaa michuano ya timu za vijana Afrika Mashariki ya Azam Youth Cup 2016 inayofikia tamati kesho Jumapili ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Timu tatu zilizoalikwa kushiriki michuano hiyo zimesema kuwa michuano hiyo itasaidia mno kukuza soka la vijana kutokana na ushindani unaoonyeshwa kwa timu zote shiriki.
Akifanya mahojiano maalumu na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Future Stars Academy, Alfred Itaeli, alisema kuwa michuano hiyo ni mizuri sana na anaishukuru Azam FC kwa kuiandaa vizuri ikiwemo kuzihudumia vema timu zote shiriki.
“Maandalizi ya hii michuano ni mizuri, kila kitu kipo hapa kama mtu yoyote anahitaji, huduma ni bora sana, ni changamoto pia vijana wanajifunza kadiri mechi zinavyozidi kwenda, tumepata nafasi nzuri sana na kubwa sana na tunaishukuru Azam FC kwa hilo, yakiweza kuendelea yatasaidia vijana wengi zaidi kuonekana na kusaidia mpira wetu kwa ujumla,” alisema.
Hii itainua soka la vijana
“Kwa kweli Tanzania tuna uhaba mkubwa wa michuano ya vijana na kuwa na mpira bora lazima uanze na vijana, kwa hiyo vijana wasipopata michuano kama hii na changamoto kama hizi inakuwa ni ngumu kupata wachezaji wazuri, hata tunavyoangalia mechi za wakubwa unaona kabisa wanakosa vitu fulani ambavyo walivikosa kwa kutopewa misingi wakati wakiwa chini kama hivi, hivyo michuano kama hii itasaidia mno soka la vijana,” alisema Itaeli
Kwa upande mwingine, Itaeli alisema kuwa tayari timu yake imeanza kuzoea uwanja wa nyasi bandia wanaochezea na ndio siri kubwa ya wao kupata ushindi kwenye mchezo wa jana dhidi ya Ligi Ndogo ya Kenya.
“Mechi ya kwanza dhidi ya Azam Academy tulikuwa na uoga na wachezaji hawakuuzoea uwanja, lakini leo (jana) tulibadilisha mbinu na kuwaweka sawa wachezaji na kupata ushindi huo, nimefurahishwa sana na timu yangu na hiki ndio kiwango chetu cha kila siku,” alimalizia.
Naye Kocha Mkuu wa Ligi Ndogo, Moses Gosege, alisema kuwa michuano hiyo imekuwa mizuri sana lakini akatoa ushauri kwa hapo baadaye ifanyike Agosti au Desemba ili waweze kujiandaa vema kutokana na wachezaji wao wengi ni wasomi na walifanya maandalizi ya siku tatu kabla ya kuja kupambana.
“Michuano ina ushindani mkubwa sana, hivi sasa sisi labda tutajipanga kuwania nafasi ya pili na naipa nafasi kubwa Azam Academy kutwaa ubingwa kutokana na ubora wao, na hii ni baada ya sisi kupoteza leo (jana), kwa kiasi kikubwa matokeo haya yamechangiwa na uchovu kutokana kwa wachezaji wangu,” alisema.
Mbali na timu zote kufurahia michuano hiyo ya kwanza kabisa ya vijana kufanyika nchini ikiandaliwa na klabu, pia yamefanikiwa kuwavutia mashabiki wengi ambao wamekuwa wakihudhuria kwa wingi na kufurahia viwango vikubwa vinavyoonyesha na wachezaji vijana.
Wengine wamediriki kusema kuwa burudani wanayoipata imezidi hata viwango wanavyodhuhudia kwa timu za wakubwa kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
0 comments:
Post a Comment