Argentina wameinyuka Chile mabao 2-1 katika mchezo wa fungua dimba wa kundi D wa michuano ya Copa America Centenario uliochezwa katika uwanja wa Levi huko Clara, Calif.
Argentina maarufu kwa jina la 'La Albiceleste' walikuwa bila ya nyota wao Lionel Messi kutokana kuendelea kuuguza majeraha yake ya mgongo aliyopata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Honduras uliochezwa Mei 27.
Baada ya kutokuanza vizuri nusu ya kwanza, Argentina walikuja kwa kasi ya aina yake, ambapo mnamo dakika ya 51, Angel Di Maria alifunga goli maridhawa baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Eva Banega.
Baadaye Argentina waliongeza bao la pili dakika ya 59 lililofungwa na Eva Banega baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Angel Di Maria.
Bao pekee la Chile lilifungwa kwa kichwa na Jose Fuenzalida dakika ya 90 kutokana na pasi nzuri ya Fabian Orellana na kufanya matokeo kuwa 2-1.
Kwa sasa Argentina na Panama wanaoongoza kundi D wote wakiwa na alama tatu na magoli 2 ya kufunga na moja la kufungwa huku Chile na Bolivia wakiwa hawana pointi na wamefungwa magoli 2 kila mmoja na kufunga goli moja.
Timu zote zitarudi kundini June kumi ambapo Chile watakuwa na kibarua dhidi ya Bolivia huku Argentina wakiwavaa Panama.
Dondoo muhimu.
- Mara ya mwisho kukutana timu hizi zilipata matokeo kama haya. Argentina waliifunga Chile mabao 2-1, mchezo uliochezwa mwezi March.
- Bila ya Messi, hakuna tatizo (no Messi, no problem): Lionel Messi hakucheza mchezo wa jana baada ya kuwa akiuguza majeraha yake ya mgongo. Kazi ya Banega na Di Maria iliwasahaulisha Argentina juu ya Messi.
- Di Maria afunga goli na kuli-dedicate kwa bibi yake: Di Maria alifunga goli na kunyanyua T-shirt ambayo ilikuwa na ujumbe ulioandikwa kwa mkono. Ujumbe huo ulikuwa maalum kwa bibi yake aliyefariki hivi karibuni. Baada ya mchezo huo, Di Maria alikuwa akitokwa machozi na alisema kwamba, bibi yake alikuwa ndiyo kila kitu kwake.
- Argentina na Chile walikutana katika fainali ya michuano hii mwaka jana na Chile kuibuka na ushindi wa matuta. Sanchez ndiyo alifunga penati ya ushindi kwa Chile.
0 comments:
Post a Comment