BAADA ya Yanga kufanikiwa kumteka beki wa kulia wa Simba, Hassan Kessy, Wekundu wa Msimbazi hao wamejibu mapigo kwa kumnasa kiungo mwenye sifa zote za nafasi hiyo ambaye ni mtaalamu wa kucheza namba zote kasoro kipa, Salum Telela.
Kama hiyo haitoshi, kuna uwezekano mkubwa wa Simba kumpata beki wa Yanga ambaye ni rafiki wa karibu wa Telela ambaye anaondoka Jangwani kutokana na hasira za kutengwa kwa pacha wake huyo.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana zinasema kuwa Telela mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kuhaha uwanja mzima, kupandisha timu pale inapobidi kufanya hivyo, tayari ameanza mazungumzo na mabosi wa Simba.
Na rafiki zake wa karibu wanafahamu fika kuwa msimu ujao Telela atakuwa katika jezi za rangi nyekundu na nyeupe baada ya kile kilichodaiwa kuchoshwa na uhusiano usioridhisha baina yake na kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm.
“Jamaa amesema msimu ujao atakuwa akiichezea Simba na kuna uwezekano wa kuondoka Yanga na …. (anamtaja mchezaji mwingine ambaye ni rafiki wa karibu wa Telela) kuungana naye Simba,” alisema mmoja wa rafiki wa kiungo huyo ambaye pia humudu kucheza kama beki wa pembeni.
Mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini alisema: “Tunafahamu Telela hana bahati na Yanga, pamoja na kuwa na uwezo mkubwa, lakini hawamtumii ipasavyo, sasa ngoja aje Msimbazi kwa watu wanaofahamu soka uone atakavyokuwa, lazima tumrejeshe timu ya Taifa.
Alisema kuwa tayari wameshafanya mazungumzo na Telela na kwamba wakati wowote watamaliza, tayari kwa kiungo huyo kuungana na wataalamu wengine ndani ya kikosi chao kama Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude na wengineo.
Alitamba zaidi: “Tena tuna mpango wa kumsajili mchezaji wao tegemeo ambaye ni rafiki yake Telela, mwenyewe amesema iwapo tutamsajili atamshawishi aje naye. Tumesikia hajakubaliana na dau analotaka kupewa na Yanga, hivyo tutatumia mwanya huo kumsajili.”
Telela alipotafutwa jana ili kuzungumzia suala hilo, muda wote simu yake iliita bila kupokewa.
Lakini habari zilizozagaa miongoni mwa watu wa karibu na Simba, zinasema kuwa baada ya minong’ono ya Telela kunukia Msimbazi, kuna kigogo wa klabu hiyo amejitolea kumsajili kwa gharama yoyote pamoja na shahidi wake ambaye ni mmoja wa wakali walioiliza APR ya Rwanda mbele ya rais wao, Paul Kagame na kuitoa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pamoja na uwezo mkubwa wa Telela, kiungo huyo amejikuta akishindwa kutamba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga, huku mara kwa mara akijikuta matatani dhidi ya Pluijm.
Iwapo Simba watafanikiwa kumsajili Telela pamoja na beki huyo, bila shaka watakuwa wamelipiza kisasi cha kuporwa Kessy ambaye alikuwa ni miongoni mwa mihimili ya Wekundu wa Msimbazi hao.
Credit:Bingwa
0 comments:
Post a Comment