UONGOZI wa Yanga upo mbioni kumpa mkataba mpya na mnono zaidi kocha wake Mholanzi, Hans van der Pluijm, baada ya kuridhishwa na mafanikio aliyoyapata akiwa na miamba hiyo ya Jangwani ndani na kimataifa.
Pluijm ambaye amefanikiwa kutawala soka la Tanzania kwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mara mbili mfululizo, amewakuna viongozi wa Yanga baada ya kuitikisa Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kuandika historia kwa kuiingiza timu hiyo ya Jangwani kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola.
Mafanikio hayo yamesababisha jina la Pluijm kutajwa na klabu kadhaa barani Afrika, kitu ambacho kimewafanya viongozi wa Yanga kuingia hofu ya kumpoteza kocha huyo aliyebakiza miezi michache kwenye mkataba wake wa sasa na kuamua kuanza mchakato wa kumfunga na mkataba mnono na wa muda mrefu.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kililiambia BINGWA kuwa tayari mabosi wa timu hiyo wapo katika mikakati kabambe ya kumpa mkataba mnono Pluijm kutokana na kazi nzuri aliyoifanya tangu alipotua kwa mara ya pili kwenye klabu hiyo kuchukua mikoba iliyoachwa na Mbrazil, Marcio Maximo.
“Kocha (Pluijm) yupo mbioni kupewa mkataba mpya utakuwa mnono zaidi kuliko yote iliyopita, hii ni kama kumpa shukrani kutokana na kazi nzuri aliyoifanya kwa vijana wa Jangwani,” alifunguka mtoa habari wetu.
Chanzo hicho kilidai kuwa viongozi wa Yanga wapo tayari kuendelea kufanya kazi na Pluijm mpaka pale mwenyewe atakapofikia kikomo na kusema basi na ndiyo maana safari hii wameamua kumwangalia mkataba wa miaka miwili au zaidi Mholanzi huyo.
Inadaiwa kuwa Yanga inataka kuachana na utamaduni wa kubadilibadili makocha ambao kwa sasa unawatesa wapinzani wao wa jadi, Simba na kubaki na Pluijm ambaye amethibitisha kuwa na uwezo wa hali ya juu kumudu soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla kitu ambacho makocha wengi wanaokuja nchini wamekikosa.
BINGWA lilipomtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdeth, ili kuzungumzia tetesi hizo za Pluijm kupewa mkataba mpya, hakukanusha wala kuthibitisha moja kwa moja taarifa hizi zaidi ya kutoa majibu ambayo yalionyesha kuna kitu kilikuwa kinaendelea.
Akizungumzia taarifa hizo, Baraka alisema: “Hilo suala sasa hivi lipo kwenye uongozi wa juu wa Yanga, muda ukifika litatolewa taarifa rasmi na mtajua kila kitu.
“Na kuhusu mkataba wa kocha siwezi kuuzungumzia kwa sababu ni siri kati ya mwajiri na mwajiriwa, hivyo nadhani sasa hivi siwezi kuzungumza mengi kuhusu suala hilo, lakini muda ukifika taarifa itatolewa tu.”
Msimu huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa Yanga chini ya Pluijm, hii ni baada ya timu hiyo kufanikiwa kutwaa taji la VPL, kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na kubwa kuliko yote ni kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa matokeo ya jumla ya mabao 2-1.
0 comments:
Post a Comment