KAMA Yanga ikifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola, beki Hassan Ramadhan ‘Kessy’, atakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na klabu hiyo kwa ajili ya michuano hiyo.
Kessy atakuwa ameangukia na ngekewa kwa kusajili katika dirisha dogo la usajili la Shirikisho la Soka Afrika CAF, utakaoanza, baada ya timu kutinga robo fainali ya michuano yake.
Beki huyo tayari amesaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa ligi kuu baada ya kumaliza kuitumia Simba ambayo alijiunga nayo akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Yanga itaingia uwanjani ikiwa na faida ya mabao 2-0, iliyopata katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kulingana na matokeo ya awali Yanga inahitaji sare ya ina yoyote au ushindi dhidi ya Esperanca, ili waweze kuingia katika hatua ya makundi na hapo ndipo beki wao mpya, Hassan Kessy, ngekewa yake itakapojitokeza.
Kwa mujibu wa sheria za mashindano hayo, timu itakayotinga hatua ya makundi inaruhusiwa kusajili wachezaji watatu wapya ili kuongeza nguvu kwenye timu zao.
Hadi hivi sasa tayari Yanga ina nafasi kubwa ya kutinga hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 wakiwa nyumbani hivyo watafaidika na usajili huo kwa kumchezesha beki wao mpya wa kulia Kessy waliyemsajili hivi karibuni.
Awali Kessy alikuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo wao dhidi ya Toto Africans, lakini baadaye Wanamsimbazi nao walimfungia michezo mitano.
Simba walifikia maamuzi hayo baada ya kudaiwa kuwa kitendo cha Kessy kupewa kadi nyekundu kimeigharimu timu jambo lililotoa nafasi kwa Yanga kumalizana naye kufuatia mkataba wake kufika ukingoni mara baada ya kumalizika msimu huu.
Credit:Bingwa
0 comments:
Post a Comment