Ni stori yenye fundisho kubwa sana. Katika maisha ya binadamu kuna mambo mengi sana ya kujifunza. Kuna kipindi cha mafanikio na wakati wa mpito ambapo mambo huwa hayaendi kama unavyotarajia. Hii inaweza kutokea katika nyanja mbalimbali za maisha kama michezo, maofisini na kadhalika.
Katika pita pita zangu nimekutana na picha ya Fernando Torres akiwa pamoja na Diego Simeone wakati huo wakicheza pamoja kunako klabu ya Atletico Madrid. Mwaka 2005 wakati huo Torres akiwa bado bwana mdogo alikuwa ndiye nahodha wa kikosi hicho na kumwongoza Simeone ambaye kwa umri alikuwa kamwacha mbali sana. Kwa kauli rahisi kabisa Torres almaarufu kama El-Nino alikuwa bosi wa Simeone almaarufu kama El-Cholo kwa wakati huo. Alikuwa na uwezo wa kupendekeza nani acheze na nani asicheze.
Ni takriban miaka 11 sasa imepita tangu Torres na Simeone wacheze pamoja. Baada ya Torres kuwa ameshapita kwenye vilabu vya Liverpool, Chelsea na AC Milan na kurudi tena Atletico. Anamkuta Simeone ndiye kocha mkuu, tena kubwa zaidi ndiye aliyesababisha ujio wake kutokana na kuzingatia mapenzi ya dhati aliyonayo kwa klabu hiyo bila ya kusahau mapenzi ya dhati ya mashabiki wa timu hiyo kwa Torres.
Ikumbukwe tu Torres ni kama alikuwa ameshapotea kwenye soka, baada ya kutoka Liverpool na kwenda Chelsea ndipo maisha yake ya soka yalipoanza kuingia dosari baada ya kupoteza imani kwa mashabiki kutokana na uwezo wake wa kufunga kuporomoka kupita kiasi. Akiwa Chelsea alifunga mabao 20 katika michezo 110 kabla ya kutolewa kwa mkopo kwenda AC Milan ambapo huko napo mambo yalienda ndivyo sivyo baada ya kufunga bao moja tu katika michezo 10.
Jinamizi hilo halikuwa zuri kwake hata kidogo, ilifikia wakati hata klabu ndogo zisingehitaji hata huduma yake kutokana na ubutu alikuwa nao mbele ya lango. Lakini licha ya yote hayo kutokea Simeone hakuona kama kuna tatizo kubwa kwa nyota huyo na kuamua kumrejesha mwaka 2015 na taratibu akaanza kurudi kwenye kiwango chake.
Leo hii tunamzungumzia Torres mwingine kabisa, Torres anayekaribia ubora wake nyakati zake za Liverpool, Torres mwenye uwezo wa kuleta madhara langoni mwa timu pinzani muda wowote. Ameaminiwa na amerudisha imani kwa kocha wake. Ametoa mchango mkubwa sana kwa timu yake kufika hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa ambapo watapambana na mahasimu wao wa jiji la Madrid, Real Madrid.
Simeone anabaki kuwa mtu mwenye historia ya kipekee kwenye maisha ya Torres. Itakumbukwa tu kwamba katika kipindi chote ambacho Torres aliitumikia Atletico kabla na wakati akiwa nahodha kati ya mwaka 2001-2007 kabla ya klutimkia Liverpool, Atletico Madrid hawakuwahi kupata ushindi mbele ya Real Madrid. Zaidi ya hapo alipata wakati mgumu hata kuwafunga mahasimu wao na ilimchukua takribani dabi nane kuwafunga ambapo hata hivyo bado hawakufanikiwa kuibuka na ushindi, hiyo ilikuwa ni katika msimu wa 2006/07 ambapo ndio ulikuwa msimu wale wa mwisho klabuni hapo. Lakini akiwa chini ya Simeone wamepata ushindi mfufulizo mbele ya Madrid tena yeye akiwa miongoni mwa wauaji wa wapinzani wao.
Nawaza tu kama Torres enzi zake akiwa nahodha wa Atletico asingemfanyia vitu vya kiungwana Simeone, je Simeone leo angeweza kumrejesha Atletico?, na hata kama angemrejesha angemwamini tena na kumpa fursa adhimu ya kusimama katika safu yake ya ushambuliaji?. Mwaka 2005 Simeone alitekeleza alichosema Torres uwanjani lakini mwaka 2016 Torres anatekeleza maagizo anayopewa na Simeone uwanjani.
Hapa ndipo utaiamini moja ya nukuu za rais wa Zimbabwe Robert Mugabe pindi aliposema “Treat every part of your towel nicely because the part that wipes your buttocks today will wipe your face tomorrow” akiwa na maana ya kwamba; ‘Tunza vizuri kila sehemu ya taulo lako kwa sababu sehemu ya taulo ambayo imefuta makalio yako leo, kesho itafuta uso’.
Kwa mantiki hiyo basi, May 28 Torres atakuwa na kazi kubwa pale ambapo atahitajika kwa juhudi zote kulipa fadhila kwa Diego Simeone kwa kuhakikisha anaipa ushindi Atletico mbele ya Real Madrid, ushindi ambao utakuwa ni ushujaa kwao wote wawili kutokana na jinsi historia yao inavyoelezea.
Kila la heri Fernando Torres (El Nino), kila la heri Diego Simeone (El Cholo).
0 comments:
Post a Comment