KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Stewart Hall, amefurahishwa na mshambuliaji wake, Allan Wanga kufuatia bao la ushindi alilofunga kwenye mechi dhidi ya Panone iliyofanyika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi jana.
Wanga alifunga bao hilo dakika ya 77 na kuifanya Azam FC kupata ushindi muhimu wa mabao 2-1 ugenini na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), bao jingine la Azam FC lilifungwa na beki kisiki Pascal Wawa dakika ya 64.
Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Hall alisema Wanga hajafunga bao kwa muda mrefu na kudai kuwa amefurahishwa naye sana hasa baada ya kuipatia ushindi muhimu Azam FC licha ya mazingira magumu waliyokutana nayo katika mchezo huo.
Mara ya mwisho Allan Wanga kuifungia bao Azam FC kabla ya jana ilikuwa ni Septemba mwaka jana alipofunga bao la uongozi wakati mabingwa hao wakiichapa Stand United mabao 2-0 mjini Shinyanga.
“Mechi ilikuwa ngumu sana, Panone walipambana kwa nguvu sana na nawapongeza kwa hilo, tatizo kulikuwa na upepo mkali sana na uwanja pia ni mbaya sana, hivyo ilikuwa ni ngumu sana kucheza mpira, uwanja ulituharibia kila kitu na ulitufanya tubadili baadhi ya mambo tuliyopanga wakati wa kipindi cha pili.
“Lakini furaha yangu kubwa nashukuru tumeshinda mchezo huo, unajua kwenye mechi ya kombe (FA Cup), ushindi wowote ni mzuri, cha muhimu ni ushindi na kusonga mbele kwa raundi ijayo na si juu ya kiwango, hivyo nina furaha kubwa kutimiza hilo,” alisema Hall.
Mwingereza huyo aliongeza kuwa wamekuwa wakifanyia sana mazoezi namna ya kupiga mipira ya kona na adhabu ndogo na kubwa analoshukuru ni mabao yote waliyofunga jana yametokana na kona.
Akizungumzia mabadiliko waliyofanya kipindi cha pili na Azam FC kurejea mchezoni, Hall alisema: “Tulipofanya uchaguzi wa kikosi cha mchezo huo, tulipanga kuwapumzisha wachezaji wetu muhimu kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Yanga, lakini tulibadili mipango yetu kipindi cha pili baada ya kutocheza vizuri, tuliwaingiza Sure Boy (Salum Abubakar), Migi (Jean Mugiraneza) na Kipre Tchetche na wote wakaleta mabadiliko.”
Wakati huo huo, kikosi cha Azam FC kimewasili salama jijini Dar es Salaam saa 6 mchana huu kwa usafiri wa ndege ya Shirika la Fast Jet kikitokea jijini Arusha, ambapo kesho saa 2.30 asubuhi kitaanza mazoezi rasmi ya kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Yanga utakaofanyika Uwanja wa Taifa Jumamosi hii.
0 comments:
Post a Comment