
KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm kwa sasa hataki kubughudhiwa kwa sababu yuko bize akifukunyua na kuzisoma mbinu za wapinzani wake Al Ahly kuelekea katika mchezo wa kwanza wa 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu hizo utakaopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Aprili 9 mwaka huu.
Mholanzi huyo amesema amekuwa akitumia muda wake mwingi kuwasoma Al Ahly kwa kutumia mikanda ya video ambayo ameipata katika michezo yao iliyopita na inayoendelea kuchezwa ili aweze kuwapa mbinu za ziada vijana wake kabla ya kukutana na miamba hiyo ya Misri.
Akizungumza na BINGWA, Pluijm alisema yuko ‘bize’ hivi sasa akiendelea kuisoma mikanda ya wapinzani wao hao katika kipindi hiki, jambo ambalo limemfanya aingie chimbo huku zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kukutana na mabingwa hao wa kihistoria wa Afrika.
“Rafiki yangu niko bize najua nini unataka, lakini ukweli kwamba natafuta mikanda ya kikosi cha Al Ahly na kusoma mifumo kabla ya kwenda kuwapa mbinu vijana kuelekea katika mchezo wetu unaofuata wa Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema.
Kocha huyo aliongeza kusema kuwa ili kuwatoa Al Ahly anahitaji muda wa kutosha kuisoma miamba hiyo ya Misri ili atengeneze mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mechi mbili ambazo zitachezwa Aprili 9 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Aprili 19 nchini Misri.
Pluijm amesema mpaka sasa tayari amenasa mbinu kadhaa za miamba hiyo Misri na bado anaendelea kutafuta mikanda yao tayari kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo la kukata na shoka ambalo linasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment