
AZAM sasa inapiga akili ndefu kujiuliza ifanye vipi kutoka kwa Esperance ya Tunisia, lakini Kocha Mkuu wa Bidvest Wits, Gasvin Hunt amefichua siri moja ya kutolewa kwao, huku akiwapa ushauri wa bure wapinzani wao kama wanataka kusonga mbele.
Kocha Hunt alisema kutolewa kwao na Azam ni mpango wao kwa sababu wanaona mashindano ya Kombe la Shirikisho hayana faida kubwa kwao, jambo lililomlazimu kutowapanga wachezaji wa kikosi cha kwanza.
Hunt alisema Azam ni timu nzuri, lakini inatakiwa sasa kujipanga vyema kuwavaa Esperance ambao anaamini hawatafuata mkondo wao wa kupanga kikosi cha pili.
Kocha huyo anaamini Watunisia hao wataishukia Azam na mziki kamili, kitu ambacho ni lazima Wanalambalamba wajipange kwelikweli ili wasikwame.
Hunt alisema Esperance ni timu nzuri ambayo ina malengo makubwa na mashindano hayo ya CAf ambapo kwao hawadharau mechi yoyote, hivyo kuitaka Azam iwe tayari kukabiliana nao la sivyo inaweza kung’olewa na kukwama kufika mbali.
“Hatukutaka kucheza mashindano haya, tulijifunza kwa Orlando Pirates walitumia kiasi kikubwa cha fedha kufika fainali mwaka jana, lakini kiasi hicho walichotumia wanaweza kukipata pale kwetu Afrika Kusini ukiwa bingwa sasa utaona hiyo tofauti ndiyo maana mnaona tumetumia timu dhaifu,” alisema Hunt.
“Azam ina timu nzuri kuna baadhi ya wachezaji nimefurahi kuona viwango vyao kama yule beki namba tano (Pascal Wawa), lakini sasa wanatakiwa wajipange kama kweli wanakutana na Esperance wasidhani watakutana na timu dhaifu kama yetu.”
Azam ilifanikiwa kuitoa Bidvest Wits kwa jumla ya mabao 7-3 baada ya kuifunga nyumbani kwao kwa mabao 3-0 kabla ya juzi Jumapili kuilaza tena mabao 4-3. Katika mchezo huo Azam hata hivyo ilionekana kujisahau kila walipokuwa wakifunga bao kwani wapinzani wao walirejesha jambo lililowatibua makocha wa timu hiyo.
0 comments:
Post a Comment